23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Tumeuchoka wimbo wa mimba’-Ndalichako

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameshangazwa na Maafisa Elimu kutoa takwimu za  wanafunzi wa kike  ndio wanaongoza kwa kuacha masomo kutokana na kupata mimba wakati  takwimu alizonazo wanafunzi wa kiume ndio  wanaongoza kwa kuacha masomo na kwenda kufanya biashara.

Pia, amewataka Maafisa hao kusimamia ubora wa elimu unaotolewa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Maafisa Elimu wa Taaluma, Michezo, Utamaduni, Elimu Maalum na Takwimu wanatimiza wajibu wao.

Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 21, jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa saba wa Chama cha Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya (REDEOA).

Prof. Ndalichako amesema takwimu alizonazo zinaonesha kwamba wanafunzi wa kiume wengi ndio wanaoacha masomo na kwenda kufanya biashara lakini kila siku maafisa elimu wamekuwa wakitoa takwimu za mimba za wanafunzi wa kike.

“Naomba tuwaheshimu watoto wa kike baadhi ya kauli zinazotolewa zinakuwa hazina afya na zinakuwa ni za udhalilishaji kwani ni watoto wetu hata wale wanaopata ujauzito tuwaone kama binadamu kwa sababu wakati mwingine kauli zinazotolewa hazipendezi na niwaombe Maafisa elimu, kuna takwimu za kutoa, kila siku mimba tu inakuwa kama vile hakuna kitu.

“Takwimu zangu zinanionesha watoto wa kiume ndio wengi wanaoacha masomo na takwimu hizi zinatoka kwenu sasa kama zimechakachuliwa mmezileta nyinyi hasa katika maeneo ambayo ni ya wavuvi na wafugaji unaona saa za shule wanauza kwenye mabasi wale kwani hamuwaoni?.

“Naomba tusimamie elimu yetu tunaposimamia watoto wanaocha shule tuangalie makundi yote na kutafuta sababu kama suala la mimba tunaendelea kujenga mabweni. Naomba sana unakuta takwimu ni mimba tu kama vile hakuna kitu kingine hiyo single(Nyimbo) yenu ya mambo ya mimba tumeichoka hii awamu ya tano mje na single(wimbo) nyingine. kila siku wimbo mmoja serikali ya Magufuli(Rais Dk. John Magufuli) ipo imara,”amesema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema sekta ya elimu inafanya kazi vizuri lakini yeye anataka wafanye vizuri zaidi ikiwa ni pamoja kuwasimamia Maafisa elimu wote waliopo katika maeneo yao kuhakikisha wanatenda kazi ambayo wanatakiwa kuifanya.

“Tunafanya vizuri lakini tunataka tufanye vizuri zaidi kwahiyo kila mmoja akawajibike. Nataka mkaweke mfumo thabiti wa kuwasimamia, waweze kuwajibika, Afisa elimu utamaduni akawajibike afisa elimu taaluma akawajibike, takwimu akawajibike, nadhani katika sekta ambayo imepewa watumishi wengi ni pamoja na sekta ya elimu.

Pia amesema serikali imejipanga kuhakikisha inazidi kuboresha masomo yote yanawajengea uwezo wanafunzi  kwenye maisha yao ya  kawaida kama masomo ya kilimo.

“Tutahakikisha tunaendelea na masomo ya michepuo kwa sababu wakimaliza tayari wanakuwa fundi mchundo na ni mtaalamu wa kushona nguo awe na utaalamu wa kilimo naamini tutayatekeleza uchaguzi umeisha sasa ni kuchapa kazi,”amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu Maafisa Elimu Wilaya kwa kudai kwamba serikali imeisha agiza magari 184 kwa ajili yao ambapo mpaka ifikapo Januari 15, 2021 yatakuwa yameishafika nchini.

“Serikali hii haina ahadi hewa nawaomba wanaohusika na manunuzi wanapoanza mwaka Maafisa elimu wawe na magari yao kuweza kufika maeneo mbalimbali,”amesema Prof.Ndalichako.

Aidha,Waziri Ndalichako amewataka Maafisa elimu hao kusimamia elimu maalum kwani ni kundi ambalo linahitaji kusaidiwa kwani kundi hilo ni wachache.

Sehemu ya Maafisa Elimu

“Jambo lingine nawaomba tusimamie  elimu maalum na ninaomba mjitume zaidi kwani bado kuna chagamoto zipo kuna baadhi ya  Wilaya zinafanya vizuri na zingine zinafanya vibaya wale wenye mahitaji maalum wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la kipekee. Ni jukumu la serikali kuwasaidia na watu wenye ulemavu tunawapa mikopo kwa asilimia 100.

Amesema serikali ipo katika mpango wa kujenga shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ya Viziwi katika eneo la Lukuledi mkoani Mtwara.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako amesema serikali imefanikiwa kupata mkopo wa Sh trilioni 1.2 kutoka benki ya dunia ambazo zitatumika kujenga shule mpya za sekondari 1,000 pamoja na shule za kidato cha tano na sita 26 kwa ajili ya masomo ya Sayansi kwa watoto wa kike.

“Tunatarajia kujenga  shule kwa ajili ya  kidato cha sita 26 kila mkoa utakuwa na shule maalum kwa ajili ya masomo ya Sayansi pia tutapanua  shule kongwe 50 ili kuongeza udahili tutahakikisha tunakamilisha vyumba vya maabara,”amesema Prof. Ndalichako.

Amewataka kuboresha elimu ya watu wazima kwani ni eneo ambalo linahitaji uhamasishaji mkubwa ndio maana serikali imeweka mfumo usio rasmi ili kuwawezesha waliopoteza sifa kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na ukosefu wamagari kwa Maafisa elimu Wilaya, upatikanaji wa vitabu wa ziada na kiada na pamoja na upatikanaji wa walimu wa masomo ya kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles