- Mkuchika asema ataanza kushughulika na viongozi, polisi wanaokurupuka kuweka watu ndani
RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SERIKALI imesema kasi ya viongozi kutoa taarifa zao kupitia fomu ya matamko ya mali na madeni ni nzuri huku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe akitajwa kuwa ni mfano wa kuigwa katika zoezi hilo.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha 2018 jumla ya viongozi 15,303 walirejesha fomu za maadili ambao ni sawa na asilimia 98 ya viongozi 15,552 ya viongozi waliotakiwa kurejesha fomu hizo.
Pia Serikali imewataka viongozi ambao wanarejesha fomu hizo kuhakikisha wanazipeleka wenyewe ili kulinda siri zao.
Hayo yalielezwa jana Jijini hapa na Kamishina wa Tume ya Maadili ya viongozi wa umma, Harold Nsekela wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Aidha,alisema kila tarehe ya mwisho ya mwezi Desemba huwa ni lazima kwa viongozi wa umma kutoa taarifa za madeni na mali zao jambo ambalo wengi wamekuwa wakilitekeleza kwa kusukumwa.
MBOWE ATAJWA
Kamishna huyo alisema Mbowe ni mmoja ya watu wanaotakiwa kuigwa katika zoezi la urejeshaji wa fomu za maadili ya umma.
Alisema licha ya kiongozi huyo kuwa Gerezani lakini aliandika barua akiomba mara baada ya kutoka ndio apeleke taarifa zake.
“Nitawapa mfano hai mnajua kwamba Mbowe kuna wakati alikuwa ndani wakati matamko haya yanarudishwa lakini alipokuwa ndani kule rumande alituandikia barua kwamba jamani siwezi kurejesha hiyo fomu kwa sababu sehemu niliyopo siwezi kuandika tuliipokea.
“Alipotoka alijaza tamko akatuletea,nadhani mmenielewa alituandikia barua tukaipokea alipotoka,”alisema
Alisema kwa mujibu wa sheria, ni kosa kwa kiongozi kutojaza fomu za maadili kwani jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria hivyo wanaoshindwa kurejesha, wanakuwa wamekiuka maadili.
ATAKA WAREJESHE KWA MKONO
Vilevile Kamishana huyo aliwataka viongozi mbalimbali ambao wamekuwa wakirejesha fomu hizo wazirejeshe wenyewe kwa mkono ili kutunza siri.
“Kwa hiyo unatakiwa wewe mwenyewe kiongozi ndio ulete hilo tamko na ninashauri ulete kwa usalama wa siri zako lile tamko ni la kwako kiongozi unachoandika mule ‘information’ ni za kwako kama kutakuwa na ukiukwaji wewe ndio utawajibika.
“Wewe kama kiongozi unampa mtu mwingine kwa usalama wako lete mwenyewe siri zikivuja utamlalamikia nani utakuja kwetu kusema zimevuja? Viongozi wenzangu naomba pokeeni ushauri leteni wenyewe ili kutunza siri,”alisema.
MKUCHIKA NA VIONGOZI KUWEKA WATEULE WA RAIS NDANI
Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora, George Mkuchika alisema maadili kwa viongozi ni jambo lisilohitaji mjadala kwani Serikali imeendelea kuwa macho na kuwamulika wote ambao wanakiuka maadili.
Mkuchika pia alisema kuna baadhi ya watu wanashindwa kutumia nafasi zao na badala yake wamekuwa ni watu wa kuwaweka ndani viongozi wa ngazi za chini jambo ambalo amekuwa akilipigia kelele.
“Kwa sasa tunaanza kuwashughulikia hata polisi ambao wanakubali kuweka watu ndani, hivi unawezaje kukubali kiongozi amuweke ndani mtu bila kukupa maadishi, nawaambia tutawashughulikia watoa amri na wale polisi ambao wanakurupuka na kuwaweka watu hao,” alisema Mkuchika.
MPANJU NA UFUKUZAJI WATU
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amos Mpanju, alisema suala la watu kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu siyo jambo jema lakini akatetea maamuzi ambayo hutolewa na Rais kwa kuwatumbua watu kwamba yupo sahihi.
Mpanju alisema ili mtu afukuzwe ni lazima kuwepo na sababu na nafasi ya kusikilizwa kwanza, lakini kwa kiongozi mkuu wa nchi hilo ni jambo la kawaida maana ndiyo mwenye uamuzi wa mwisho.