32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tuhuma za mizengwe zaibuka Uchaguzi wa amani Msumbiji

MAPUTO, MSUMBIJI

ZOEZI  la kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji  licha ya kufanyika kwa amani, limegubikwa na tuhuma za mizengwe, ikiwamo  kuwapo kwa masanduku yaliyojazwa karatasi za kura zilizopigwa hata kabla ya uchaguzi kuanza. 

Shirika moja la kiraia limeripoti visa hivyo, na matukio mengine ikiwamo watu kadhaa waliokamatwa na kadi zaidi ya moja za kupigia kura. 

Shirika hilo liitwalo Center for Public Integrity, CIP lilinukuliwa na shirika la habari la DPA, likisema visa hivyo vya kughushi vililenga kukipendelea chama tawala cha Frelimo. 

CIP lilisema katika baadhi ya maeneo ambayo ni ngome za Frelimo, waangalizi huru wa uchaguzi walizuiwa kufanya kazi yao. 

Uchaguzi huu unachukuliwa kuwa muhimu kwa utengamano wa Msumbiji, baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na vimbunga vibaya vilivyoikumba nchi hiyo mwanzoni mwa mwaka huu. 

Uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa chama kikuu cha upinzani, Renamo, kinaweza kushinda majimbo matano kati ya 11 ya nchi hiyo.

Kuna mikoa 11 ambayo imetajwa kuwa ni karata muhimu iliyobadilisha mambo katika uchaguzi huu ambapo imeshuhudiwa chama cha Upinzani kitakuwa na fursa ya kuchagua magavana katika mikoa ambako wanashinda kura nyingi zaidi.

Ikumbukwe kwamba hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 40 ya utawala wa chama cha Frelimo,upinzani unapata nafasi hii ya kuchagua magavana kwenye mikoa hiyo.

Tayari tuhuma hizo zinatajwa kuitia dosari Msumbiji.

Rais Phillipe Nyusi juzi wakati akipiga kura yake alisema huu ni uchaguzi unaofuatiliwa sana kuliko mwingine wowote nchini Msumbiji ,katika kanda hiyo na pengine Afrika kwa ujumla.

Lakini mgombea urais kutoka  chama kikuu cha upinzani Renamo, Ossufo Mamade alitoa wito kwa Nyusi kukubali uwezekano wa kushindwa kwenye uchaguzi huu na kuwatia moyo wanamgambo wa chama chake kutohujumu uwazi katika mchakato huu.

Mgombea huyo wa Renamo anasema chama chake hakitokuwa tayari abadan,asilan  kukubali  matokeo ya uchaguzi ya udanganyifu na kuongeza kutoa onyo kwamba kuwanyima ushindi waliowengi  kutaipeleka nchi hiyo kwenye uhasama wa kijeshi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Takribani watu milioni 13 wamejiandikisha kupiga kura kati ya raia milioni 30 wa nchi hiyo. 

Shughuli ya kuhesabu kura imeanza na matokeo ya mwanzo yanatarajiwa kutangazwa leo Alhamisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles