28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO| Ole wenu Chadema!

Kama ilivyo ada na shauku yangu kwa miaka mingi sasa tangu mwaka 1992, nimekuwa mfuatiliaji wa siasa za ushindani katika nchi hii.

Kwa sasa shauku yangu kuu, iliyodumu kwa zaidi ya miaka 20 imekuwa kuisoma na kujifunza kila wakati kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lazima niwe mkweli, shauku hiyo kwa kiwango kikubwa ilijengwa na maneno aliyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Chadema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Sina sababu ya kuyarejea, hapa kwa sasa.

Sababu kuu ya pili ya kuifuatilia Chadema iliendelezwa kwa kiasi kikubwa na kazi aliyoanza kuifanya, Freeman Aikaeli Mbowe katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 na 2005 alipokuwa Mbunge wa Hai kwa tiketi ya chama hicho, hata kabla hajachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema mwaka 2004.

Viongozi wa Chadema wakiwa kwenye picha ya pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Sababu ya tatu ya shauku yangu ilijengwa katika misingi ya kukatishwa kwangu tamaa na kuharibika na kuharibiwa kwa kazi ya kutukuka iliyoanza kufanywa na viongozi wakuu wa mwanzo wa mageuzi nchini akina Mabere Marando, Dk. Masumbuko Lamwai, James Mbatia, Ndimara Tegambwage na wenzao kadhaa ndani ya chama cha NCCR Mageuzi.

Kwa sababu ya shauku hiyo, kila wakati nimekuwa nikipatwa na mhemuko mkubwa wa kifikra na pengine hamasa ya kujiingiza katika minyukano ya kichambuzi ninapoona kuwapo kwa jitihada za baadhi ya mashujaa wapya wa demokrasia wakifanya mashindano yanayofanana na ujinga uliopata kufanywa na waasisi wa mageuzi nchini ambao wala sipati shida kuandika tena leo, ndiyo umekuwa mpenyo na turufu ya CCM kubakia madarakani.

Katika kufanya hivyo, mara kadhaa nimejitahidi kuikana nafsi yangu, hata kujaribu kujitwika ‘magunia ya misumari kichwani’ ilimradi tu nifanye kile ninachoamini kinaweza kunusuru ustawi wa demokrasia shindani nchini.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana nimeona ni busara leo kuipa Chadema ‘ole’ kwa sababu ya kile ninachokiona kikiendelea kutokea ndani ya chama hicho.

Kwa namna ile ile ilivyopata kuwapo kabla, nachelea kuandika kuiasa Chadema kukwepa mtego wa kiburi na jeuri ya mafanikio iliyotokana na ukubwa na uzuri wa kazi mliyofanya kwa miaka mingi, mkaendekeza hulka za ubinafsi za kusaka vyeo na kuchonganisha viongozi wenu wakuu.

Kinachoendelea kufanyika sasa ndani ya Chadema na kushabikiwa na makundi hasimu ndani na nje ya chama hicho iwapo kitaachwa kistawi kabla ya viongozi wake kukaa chini na kutafakari, basi tutarajie kile kilichowapata NCCR Mageuzi kati ya mwaka 1995 na 2000 na baadaye CUF kati ya 2015 na 2020 kitawafika ninyi pia.

Lazima tuwe wakweli, Chadema iko hapa leo kwa sababu ya kazi kubwa, ngumu na hatari iliyofanywa na viongozi na wanachama wake na imegota hapo ilipo kama chama kikuu cha upinzani kwa sababu pia ya makosa yake.

Kwamba Chadema imejijenga na wakati huo huo ikajibomoa au kubomolewa na CCM ni ukweli wa kihistoria.

Kwamba Chadema ndiyo chama kikuu cha upinzani kwa sasa kwa upande wa Tanzania Bara wala hilo halina ubishi.

Kwamba Chadema kupitia UKAWA ilishiriki kikamilifu kwa namna ile ile alivyofanya Rais Jakaya Kikwete kukwamisha mchakato wa kwanza wa mabadiliko ya Katiba huo ni ukweli mchungu pia.

Kwamba Chadema mmeshindwa kila wakati kutumia fursa ya ukinara wenu kuunganisha nguvu na kuulinda kwa mbinu za medani mshikamano wa kudumu wa kambi ya upinzani tangu mwaka 2005, pamoja na ukweli kwamba kumekuwa na jitihada za namna hiyo, hilo pia linapaswa kuwa darasa la ninyi wenyewe kuwa walimu na wanafunzi.

Ni bahati mbaya kila wakati ndani ya Chadema anatokea mtu au kikundi cha watu cha kujaribu kutikisa hali ya ustawi wa chama chenu tangu zama za akina Paul Kyara, baadaye Amani Kaburu, Zitto Kabwe na wenzake na mwisho Dk. Slaa.

Dk. Willbrod Slaa.

Mlio ndani ya Chadema leo, naona kuna mtu au watu wanajaribu kufanya makosa yale yale ya kilevi na kijinga ya akina Kyara, Kaburu, Zitto, Dk. Slaa na wengine huko nyuma.

Laiti kama uongozi Chadema ungechukua hatua madhubuti si tu ya kudhibiti uasi ndani ya chama hicho bali kutafuta mwafaka wa kiuongozi na kimaamuzi kila wakati kunapotokea nyufa zinazodai marekebisho na ukarabati, pengine leo, taswira ya kidemokrasia isingefika hapo ilipo leo.

Leo hii ustawi wa Chadema kama chama kikuu cha upinzani unalo baka moja la kuwapo kwa ACT Wazalendo, chama ambacho jeuri ilichonacho leo ni matokeo ya makosa ya kiuongozi ya ndani ya Chadema ulianza kwa kuwafukuza ndani ya chama hicho akina Zitto Kabwe na Profesa Kitila Mkumbo mwaka 2014.

Hivi nani hajui kwamba mparanganyiko ndani ya CUF mwaka 2015 japo ulikuwa na mkono wa CCM, sababu ya msingi ilikuwa ni kuimarika zaidi kwa nguvu za kiuongozi ndani ya Chadema?

Hivi ni mchambuzi gani huru na makini asiyejua kuwa, Lipumba ‘alinunulika’ akahadaika kwa mfano ule ule wa Dk. Wilbroad Slaa kwa sababu ya kishindo cha Chadema kilichowaingiza ulingoni mawaziri wakuu wawili wastaafu kwa mpigo wakati wa mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?

Hivi ni mwanademokrasia gani makini asiyekumbuka kwamba yalikuwa ni makosa makubwa kwa Chadema kukaa mbali na akina Maalim Seif Sharif Hamad, Juma Haji Duni, Ismael Ladhu Jussa na wenzao waliokuwa CUF wakati walipohitaji sana sana kujiunga na Chadema baada ya mkwamo waliokutana nao wakiwa CUF.

Kama si uhafidhina wa siri siri na jeuri ya mafanikio ndani ya uongozi wa Chadema, leo hii Chadema ndiyo kingekuwa chama kikuu cha upinzani katika pande zote mbili za muungano.

Ninaweza nikasema kwa kujiamini kabisa kwamba, viongozi wakuu wanne wa Chadema; Freeman Mbowe, Tundu Lissu, John Mnyika na Salum Mwalimu wamekuwa ni watu wenye heshima na ushawishi mkubwa wa kiuongozi Zanzibar, ingawa kwa bahati mbaya tu wako upande wa wachache wanaiipinga CCM visiwani humo.

Kwamba Chadema ilifanya makosa makubwa ya kiuongozi ya kuwaacha wana CUF Masalia waliokuwa wakikihitaji Chadema zaidi kuliko chama kingine chochote cha upinzani kuungana nacho waende ACT Wazalendo kwa shingo upande kwa sababu tu za kimakosa ya viongozi wenye hulka za kihafidhina Chadema ni jambo la kujifunza zaidi kuliko kujutia au kurejea makosa yale yale.

Nachelea kuandika pasipo shaka kwamba, Chadema inayoendelea kujiimarisha kila wakati, inaendelea kufanya hivyo wakati ule ule ikiendelea kujistawisha katika misingi ile ile ya kukataa kujifunza kwa makosa ilihali ikiingia katika mitego ile ile ya kushindwa kulinda ustawi wake na mafanikio waliyopata kwa kujenga mshikamano na umoja wa kweli hasa miongoni mwa viongozi wakuu wa vyama hivyo.

Yaliyopita si ndwele, tugange ya sasa na yajayo.

Baadhi yetu ni mashabiki na marafiki wa ustawi wa demokrasia ya kweli na mafanikio halisi na ya kushangilia ya vyama vya ushindani (msisitizo ‘ushindani) kuliko ilivyo kwa vyama vyenyewe.

Kuna kila dalili za wajinga kadhaa sasa kupenyeza chokochoko za kuwagawa viongozi wakuu wa Chadema.

Kwa bahati mbaya miongoni mwa mateka wa ajenda hizo wako pia viongozi wenye majina makubwa ndani ya chama hicho.

Wanaofanya hivyo wanaweza wakawa ama wanajua wanachokifanya au wanafanya kishabiki pasipo kujua matokeo ya ujinga wao huo ambao madhira yake si tu kwamba yataishia Chadema bali yatarejesha nyuma kwa mara nyingine tena, si ya kwanza au ya pili au ya tatu ya kuimarisha ustawi wa demokrasia halisi ya ushindani wa vyama vingi.

Wanaoweza kulinusuru taifa katika hili ni viongozi hawa hawa maana ndiyo waliobeba dhamana ingawa ni kweli pia kwamba ni hawa hawa ambao wamekuwa vinara wa makosa yaliyotukwamisha siku zilizopita.

Kwa maoni yangu, makosa waliyofanya siku zilizopita na mengine wanayoendelea kuyafanya sasa hata kama athari zake ni kubwa lakini bado naamini kazi wanayoifanyia nchi hii ni kubwa na yenye thamani kubwa kuliko ukubwa wa makosa waliyofanya na kutukwamisha.

Si jambo au kazi rahisi kuwa nambari moja, lakini ni kazi kubwa na ngumu zaidi kubakia nambari moja.

Ole wenu CHADEMA.

Absalom Kibanda
Brain Inc. Ltd
Mei 21, 2023

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles