WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump bado anaonekana kuteswa na mtu aliyevujisha mawasiliano ya siri kati yake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky yenye nia ya kumtengenezea kashfa mpinzani wake wa kisiasa, Joe Biden anayepambana naye katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Trump amesema anataka kukutana na mtumishi wa idara ya ujasusi ambae hataki jina lake lijulikane, aliyefichua siri hiyo ya kadhia ya Ukraine.
Amesema kama ilivyo kwa raia wengine na yeye pia ana haki ya kukutana na anaemtuhumu.
Kauli hiyo ya Trump imekuja ikiwa ni siku chache baada ya mtu aliyevujisha mawasiliano hayo kubainika kuwa ni ofisa wa Shirika la Kijasusi la CIA.
Ofisa huyo wa CIA aliyemlipua Trump hadi kusababisha Congress kuanzisha uchunguzi dhidi yake ambao unaweza kumwondoa madarakani bado hajatajwa jina lakini alipata kufanya kazi Ikulu.
Trump amemtuhumu ofisa huyo kwa kueleza uwongo kuhusu mazungumzo aliyofanya pamoja na rais wa Ukraine, Senelnskyj.
Wakati Trump akitamani kumwona ofisa huyo sasa sauti iliyorekodiwa wiki iliyopita akitaka kumjua mtu aliyevujisha taarifa hizo zilijenga hofu kwamba huenda anataka kulipa kisasi.
” Ninataka kujua ni nani huyo mtu, ni mtu gani aliyempa mtu huyo taarifa. Kwa sababu huyo yuko karibu na majasusi,” alisikika Trump katika kikao chake binafsi na wafanyakazi wa Ikulu.
Akielezea kazi ilivyokuwa ikifanywa na majasusi wa Marekani zamani Trump pia amesikika akisema: ” Unajua tulichokuwa tunafanya siku za nyuma tulikuwa smart? sawa? upelelezi na uhaini, tulikuwa tukishughulikia kidogo tofauti na tunavyofanya sasa…”
Kauli hizo zililaaniwa vikali na wenyeviti wa kamati tatu za Democrat katika Baraza la wawakilishi.
Katika taarifa yao ya pamoja walisema kauli hizo ni “vitisho dhidi ya shahidi” na jaribio la kuzuia uchunguzi wa mashtaka yanayomkabili yeye Trump.
Mjumbe mmoja wa Democrat alisema anataka mtoa taarifa huyo za siri azungumze na kamati ya usalama mapema.
“Nina wasiwasi na baadhi ya kauli za rais anazozitoa dhidi ya mtu huyo aliyetoa taarifa za siri, na huenda akalipiza kisasi dhidi ya huyo mtu,” alisema Raja Kirshnamoorthi.
Wiki iliyopita Ikulu ya White House ililazimika kutoa taarifa kuthibitisha kuwa, Julai 25, Trump alimuomba Rais Volodymyr Zelenski kumchunguza Biden anayesaka tiketi ya urais kupitia chama cha Democrats, ambaye mtoto wake alikuwa akifanya kazi na shirika la gesi la Ukraine.
Kwa mujibu wa mukhtasari, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.
Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mtoto wa, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.
Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.
“Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo,” Trump ananukuliwa akisema kwenye mazungumzo hayo na kuongeza:
“Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.
“Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo…ni jambo baya sana kwangu.” Anadaiwa kusikika Trump katika mazugumzo hayo
Zelensky naye anaripotiwa kujibu”Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.
“Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana.”
Akimshukuru Trump, Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.