Al-Shabab washambulia kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Marekani

0
729

MOGADISHU, SOMALIA

KUNDI la kigaidi la al- Shabab kimetekeleza mashambulio mawili jana mojawapo ni katika kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Marekani kilichopo nchini Somalia na kusababisha madhara kadhaa.

Kituo hicho kilikuwa kinatumiwa na wanajeshi wa Marekani kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa makomandoo.

Wakazi wanaoishi karibu na eneo hilo walisema kuwa, walisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na risasi katika uwanja wa ndege wa Baledogle, kusini mwa mji wa Shabelle.

Kundi la al-Shabab limesema limefanya shambulizi hilo kwa kutumia bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari kulipua mageti kabla ya kuingiza ndani wapiganaji wake.

Kupitia taarifa yao, Al-Shabab walisema kuwa wameanzisha mashamblizi hayo na kwamba yataendelea.

“Baada ya kuvunja vizingiti vyenye silaha nzito, mashujaa wa mujahideen [wapiganaji watakatifu] walitikisa kituo hicho cha kijeshi kisicho cha kawaida, wakiwashirikisha askari wa jeshi hilo kwenye moto mkubwa,” inaeleza taarifa yao

Kituo hicho kipo kilomita 100 (mile 60) magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu, inasemekana   ni kituo cha vikosi maalum vya Marekani, vikosi maalum vya Somalia na walinda amani wa Uganda.

Tangu Rais wa Marekani, Donald Trump aingie madarakani, mara moja Marekani iliongeza mashambulizi ya anga dhidi ya al-Shabab, kundi ambalo linatajwa kuwa msharika wa kundi la kigaidi duniani la al-Qaeda.

Taarifa  kutoka kwa maofisa wa Somalia zinaeleza kuwa kundi hilo nalo limeonekana kuongeza mashambulizi mjini Mogadishu kama njia ya kulipa kisasi mashambulizi ya anga dhidi yake.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani inasema al-Shabab bado wanadhibiti eneo kubwa la Somalia na wana uwezo wa kutekeleza mashambulizi makubwa ya mabomu ya kujitoa muhanga, vifaa ya milipuko, na silaha nyingine za kisasa.

Katika tukio jingine kituo cha washauri wa mafunzo cha  Umoja wa Ulaya  nacho kimeshambuliwa na bomu la kwenye gari mjini Mogadishu.

Wizara ya Ulinzi ya Italia kupitia kwenye taarifa yake ilithibitisha  kuwa kikosi cha kijeshi cha Italia kilipigwa na mlipuko.

Hadi jana jioni hakukuwa na mtu aliyejeruhiwa ambaye ameripotiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here