JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA |
RIPOTI rasmi ya kwanza ya uchumi ya Rais Donald Trump kwa Bunge la Marekani ilidai: Uchumi unaanguka kutokana na makosa, ambayo si ya Trump bali mtangulizi wake Barack Obama.
Huyu ndiye Trump halisi vitu vinapoenda au kumwendea kombo ni mwepesi kusingizia wenzake. Ni tofauti na Obama wakati akiingia madarakani mapema mwaka 2009.
Naam, tofauti na Trump aliyeukuta uchumi katika hali nzuri, Obama aliikuta nchi ikiwa katika mdororo mkubwa wa uchumi, uliosambaa duniani hususani Ulaya.
Obama alipoingia madarakani licha ya kuwa uchumi aliukuta ukiwa umedhoofu kutokana na sera mbaya za mtangulizi wake, mbabe wa vita, George W. Bush, wakati wa kampeni alijiepusha kumtupia lawama Bush.
Kama kulikuwa na makombora ya lawama alimlenga aliyekuwa mpinzani wake John McCain na chama chake cha Republican kwa ujumla wake na si Bush binafsi.
Na hata alipoingia madarakani katika miaka ya awali Obama alipata shida kuurudisha uchumi alioachiwa na mtangulizi wake katika mstari na kusababisha mashambulizi mengi kutoka kwa wakosoaji wake wa Republican.
Lakini bado Obama hakuinua sauti kuwakumbusha wakosoaji hao kuwa ni wao Republican na Bush wao walioifikisha nchi hapo ilipo badala yake alijitahidi kuwatuliza kuwa mambo yatarejea kama kawaida.
Na iwapo mashambulizi kama hayo kwa Bush yalikuwapo basi yalifanywa na watu wengine.
Wakati Obama akionesha ukomavu huo Trump katika masuala mengi ikiwamo hili la uchumi ameonesha wingi wa utoto huku kile akizungumzacho mara nyingi kikiwa hakiakisi ukweli, huku akikataa kutambua juhudi za Obama zilizorudisha uchumi katika mstari na kutajirisha mabilionea kama yeye.
Wakati ikiwa bado mapema kuhukumu utawala wa Trump linapokuja suala la uchumi hadi pale atakapoondoka madarakani, tafiti za karibuni zinaonesha namna biashara ya Trump ilivyoendelea hadi sasa,
Hiyo inahusisha wakati Marekani ikiwa na marais walioingia madarakani kabla yake, ikihusisha pia namna kipato cha Trump kilivyo pia katika utawala wake mwenyewe.
Trump alianza kufahamika zaidi wakati wa utawala wa Rais Ronald Reagan mwaka 1981 hadi 1989 wakati alipojitengenezea dola milioni 800.
Trump na baba yake Fred waliingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya mabilionea na mamilionea ya jarida maarufu la Forbes ya watu 400 mwaka 1982 baada ya utajiri wao kwa pamoja wakati huo kuelezwa kuwa wa dola milioni 200.
Miaka michache baadaye Forbes ilimuorodhesha Donald Trump pekee kama bilionea rasmi kwa mara ya kwanza wakati wa utawala huo wa Reagan.
Utawala wa Reagan unafahamika kwa kutoa nafuu nyingi ikiwamo za kodi kwa matajiri wengi na hivyo kuwanufaisha vilivyo na kushuhudia mwaka 1988, Donald akinunua Plaza Hoteli.
Donald aliiboresha kutoka kuwa hoteli ya nyota tatu hadi ya nyota nne kwa msaada wa aliyekuwa mke wake Ivana. Donald pia alijipatia kile kinachojulikana sasa kama miliki yake ya Mar-a-Lago wakati wa utawala wa Reagan.
Katika utawala wa Rais George H. Bush (Bush Mkubwa) wa miaka 1989-1993 utajiri wa Trump kwa mara ya kwanza uliporomoka.
Ni baada ya kupoteza dola bilioni 1.7 na kutangazwa muflisi mara mbili wakati wa utawala huo, kwa mujibu wa Forbes.
Ivanka Trump aliwahi kugusia namna Donald kipindi hicho alivyotopea katika mlima wa madeni.
Alieleza pia namna wakati fulani Trump alivyomwelezea mtu asiye na makazi akisema, “Mtu yule ana bilioni 8 zaidi kuliko mimi,”
Forbes iliripoti namna kila alichofanya kilienda vibaya, mwaka 1986 kwa mfano alinunua miliki ya ufukweni mwa West Palm, ambalo hata baada ya kuiboresha, ilibakia ngumu kuiuza na ikawa mali isiyozalisha faida.
Ukaja utawala wa Rais Bill Clinton miaka 1993-2001, ambao sera zake zilikuwa nzuri kwa biashara ya Trump, ambayo ilifufuka na kuchanua tena.
Utawala wa Rais Bill Clinton ulimtengenezea fursa na faida kubwa zilizoshuhudia akijilimbikizia kipato kipya cha dola bilioni 1.7 hadi wakati Clinton anaondoka madarakani mwaka 2001.
Trump alifanya vyema mno katika soko la mali zisizohamishika, akijipatia miliki zilizokuja fahamika sasa kama Trump Tower, Trump Building na Trump Hotels & Casino Resorts (THCR).
Afya ya kiuchumi iliyoshuhudiwa Marekani wakati wa utawala wa Clinton, ilichochea ukuaji wa nguvu wa uchumi wa asilimia nne kwa mwaka na kuvunja rekodi kwa utengenezaji wa ajira nyingi hasa katika sekta binafsi.
Baada ya Clinton akaja Rais George W. Bush, ambapo Trump alitengeneza dola bilioni 1.3 wakati wa Bush mtoto miaka 2001-2009.
Mwanzo mwa utawala wa Bush wa pili ulishuhudia Trump akikamilisha mjengo ufahamikao kama Tump World Tower- si mbali na yalipo makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), likiwa jengo refu kabisa la makazi duniani wakati huo.
Trump pia alinunua iliyokuwa hoteli Delmonico na kuifungua ikijulikana kama Trump Park Avenue mwaka 2004.
Aliongeza dola bilioni 1.3 katika utajiri wake wakati wa utawala wa George W. Bush kufikia msimu wa mapukutiko mwaka 2008, licha ya kwamba mdororo mkubwa wa uchumi ulidumu kuanzia Desemba 2007 hadi Juni 2009.
Utajiri wa Trump ulishamiri zaidi wakati wa utawala wa Obama 2009-2017, kipindi alichotengeneza dola bilioni 2.9.
Kuna sababu nyingi zilizochangia kutengeneza kipato kilichovunja rekodi wakati wa utawala wa Obama, ikiwamo namna uchumi ulivyokuwa kabla ya Obama kuingia madarakani.
Kwa mujibu wa Forbes, uchumi ulikuwa shagalabala mwaka 2009 na utajiri wa Trump wakati huo ulielezwa na Forbes: Utajiri wa Trump ulirekodiwa kama dola milioni 1.6 kiwango cha chini kabisa tangu mwaka 1999.
Kufikia mwaka 2013 Trump aliivunja rekodi yake mwenyewe kwa kujilimbikizia utajiri wa dola bilioni tatu na kumfanya awe na jumla ya dola bilioni 4.5.
Akiwa ameingia madarakani mapema mwaka jana, Trump tayari hadi sasa amepoteza dola milioni 400 wakati wa urais wake huu, kitu ambacho wataalamu wa uchumi wanakihusisha na sababu kadhaa ikiwamo haiba yake kama Rais.
Nyingi ya biashara zake zilikabiliana na anguko la kifedha kutokana na wateja kususia biashara za Trump.
Taasisi nyingi za hisani zimesitisha kuendesha matukio ya shughuli mbalimbali katika Hoteli ya Mar-a-Lago. Wawekezaji wamekuwa wakikwepa makubaliano ya kibiashara yanayogusa jina la Trump katika majengo.
Hata hivyo. Licha ya namna anavyochukuliwa na vyombo vya habari, Trump bado ana wafuasi wengi. Makundi yanayomuunga mkono Trump yako tayari kuhakikisha utajiri wake hauporomoki sambamba na biashara zake.
Wafuasi wa chama chake cha Republican wako tayari kulipia huduma mbalimbali katika hoteli za Trump.
Forbes pia limeripoti Rais anaweza kuokoa dola milioni 11 kwa mwaka kutoka muswada mpya wa kodi uliopitishwa na Bunge.
Anachozungumza Donald Trump kipindi hiki cha utawala wake ni kwamba uchumi unashamiri. Anahusisha ukuaji wa uchumi na sheria ya kupunguza kodi iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge.
“Kodi zenu zimeshuka na sasa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu viwanda vinarudi na kila kitu kinarudi Marekani,” Trump alijigamba wakati wa hotuba aliyoitoa katika kampuni ya utengenezaji bidhaa jimboni Ohio. Aliongeza kuwa Marekani kwa mara nyingine iko wazi kwa biashara.