27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Trump alikoroga Marekani

trump-speakingNEW YORK, MAREKANI

HATUA ya Rais mteule, Donald Trump akiwa na Makamu wake Mike Pence na bintiye Ivanka Trumo kukutana na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, imezua mjadala miongoni mwa wanasheria nchini hapa.

Mkutano kati ya Trump na Abe ulifanyika katika jumba lake la kifahari lililopo Manhattan jijini hapa.

Hata hivyo, Trump hajaweka bayana mipango na mtazamo wake kwa Japan na nchi nyingine za Asia na ahadi zake za uchaguzi kuwafanya washirika wa Marekani kulipia misaada ya kijeshi wanayopewa na nchi hiyo.

Pia kumeibua maswali yasiyokuwa na majibu, hususani kwa nchi za Bara la Asia kwani Trump ameonyesha upinzani wake wa dhahiri dhidi ya Rais anayemaliza muda wake madarakani, Barack Obama kuhusu masuala ya kibiashara  dhidi ya nchi za Pasific.

Hata hivyo, msemaji wa Trump, amesema kwamba mkutano baina ya viongozi hao wawili ndiyo mwanzo wa utamaduni usio rasmi, kwani Rais Obama bado hajamaliza muda wake.

Aidha, msemaji huyo, Katrina Pierson, alisisitiza kuwa mkutano huo haukuwa rasmi baina ya Serikali mbili, badala yake ni kiongozi mmoja wa Serikali na mwingine mtarajiwa.

Kisheria hadi sasa Trump si Rais wa Marekani, kwani  ataanza kuliongoza taifa hilo Januari 20, 2017 mara baada ya kuapishwa.

Kiapo hicho kitafanyika baada ya kuthibitishwa kisheria Desemba 19.

Akizungumzia ziara ya Abe, Profesa Brad Williams wa Chuo Kikuu cha City huko Hong Kong, aliiambia CNN kuwa mkutano huo wa awali si rasmi, ulifanyika kama sehemu ya Serikali ya Japan kutaka hatima ya uhusiano wake na Marekani.

“Abe anakwenda kwenye mkutano wa APEC, kwa hiyo alihitaji kwenda Marekani kwa vyovyote vile ili kufahamu hatima ya uhusiano wa mataifa hayo mawili,” alisema.

Naye Koichi Nakano, mtaalamu wa masuala ya sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Sophia, aliiambia CNN kuwa utawala wa Japan umeharakisha kuonana na Trump kabla hajaingia rasmi madarakani, kwa kuwa amejikita kuunda baraza la mawaziri kwa sasa.

“Watafaidika nini na ziara hiyo? Kwa kweli sifahamu. Tungeweza kumzungumzia rais, lakini mtu hajawa rais rasmi. Kama utataka kufahamu ni kiongozi gani anapendwa na Shinzo Abe hapa duniani, utagundua anapenda viongozi thabiti kama Vladimir Putin (Russia), Narendra Modi (India) na Erdogan ambao wamekuwa imara kimsimamo katika uongozi wao. Yawezekana sasa anamwona Trump yuko kundi hilo,” alisema Nakano.

 

KUMTEUA MKWEWE KUWA WAZIRI?

Swali jingine linaloulizwa sasa ni mwenendo wa mkwe wa Trump, ambaye inadaiwa anaweza kuwa sehemu ya baraza la mawaziri atakaloliteua.

Inaelezwa kuwa Trump anakusudia kumteua mkwewe huyo, Jared Kushner, mume wa mwanawe Ivanka Trump ambaye kiasili ni Myahudi, lakini anafanya majadiliano na wanasheria ili kutovunja sheria za Marekani katika uteuzi.

Wachambuzi wanasema iwapo Trump atamteua Kushner, utakuwa upendeleo na kinyume cha sheria.

Kwa upande wake, Kushner anazungumza na wanasheria ili kupata ushauri wa namna ya kukasimu biashara zake kwa watu wanaoaminika pamoja na mishahara yao.

Suala hilo nalo linatajwa kuwa moja ya ishara za Kushner kuandaliwa uwaziri katika Serikali ijayo ya Trump.

Kwa mujibu wa sheria za Marekani, rais hatapokea huduma zozote zile ambazo hazitajwi katika sheria, pamoja kuwateua watu wa familia yake kuwa sehemu ya Serikali.

TED CRUZ ATAMANI UTEUZI

Seneta wa Jimbo la Texas, Ted Cruz, ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa Trump katika kuwania kuteuliwa urais ndani ya Chama cha Republican, amethibitisha kuwa yupo tayari kufanya kazi na rais huyo mteule.

Akizungumza kwenye mahojiano na Fox News, alisema: “Nina hamasa ya kufanya kazi na rais katika nafasi yoyote nitakayopewa, nitalinda kanuni na taratibu kwa mujibu wa uteuzi niliopewa ili kuhakikisha tunakuwa pamoja katika kulifanyia kazi taifa letu.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles