28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

CUF Mtwara wamchongea polisi Maalim Seif

maalim-seifNA FLORENCE SANAWA – MTWARA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mtwara limezuia mkutano wa ndani wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kupokea barua kutoka kwa uongozi wa CUF Wilaya ya Mtwara wakiwaomba kuchukua hatua hiyo kutokana na hofu ya kutokea uvunjifu wa amani.

Mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, uliitishwa na Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF) na kuongozwa na Maalim Seif ambaye yuko mkoani hapa kwa ziara ya siku mbili.

Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Maalim Seif alitarajiwa kuzungumzia hali ya siasa nchini chini ya utawala wa mwaka mmoja wa Rais Dk. John Magufuli.

Ziara ya Maalim Seif ni ya kwanza mkoani hapa tangu chama hicho kikumbwe na mgogoro ambao msingi wake umesababishwa na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kumrudisha Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi yake ya uenyekiti.

Kitendo cha mkutano huo kuzuiliwa na polisi ambao walizingira eneo la Ukumbi wa Chuo cha SAUT ulipotakiwa kufanyika wakiwa na gari la maji ya kuwasha na kuimarisha ulinzi, kumesababisha JUVCUF mkoani hapa kulilamikia Jeshi la Polisi kwamba linatumika kisiasa na kuwahujumu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya jeshi hilo kuzuia mkutano huo, Maalim Seif, alisema Katibu wa Wilaya wa CUF hana mamlaka ya kumzuia yeye kufanya mkutano au kuzuia mkutano wake wa kuangalia miradi ya maendeleo ndani ya chama chao.

“Hiki ni kioja cha mwaka, sijawahi kuona mahali popote duniani kikitokea, hii haiwezi kuwa ni uongozi wa CUF wilaya kwa kuwa hawana uwezo wa kuzuia mkutano huu, hapa Serikali imehusika  kukwamisha huu mkutano,” alisema Maalim Seif.

Pia alisema kitendo cha polisi kuzuia mkutano huo ni moja ya njama iliyofanywa na Serikali ya kuukwamisha jambo alilosema kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia.

Alisema chama chao kilifuata taratibu zote wakati wa maandalizi ya mkutano huo, kuanzia ngazi za juu hadi mkoa na ungefanyika kwa kufuata taratibu zote za kisheria pasipo uvunjifu wowote wa amani.

“Katibu wa CUF wilaya hana mamlaka ya kuandika barua kwa polisi ili kumzuia katibu mkuu wa Taifa asifanye mkutano, inashangaza, yaani hao watu wamefikia hatua hadi kwenda katika Ukumbi wa Chuo cha SAUT ambao nilitarajia kufanya mkutano wangu na kuzuia eti kwa sababu kuna viashiria vya vurugu jambo ambalo sio kweli,” alisema Maalim Seif.

Baada ya mkutano huo kuzuiliwa, Maalim Seif na uongozi wa chama hicho walikwenda mkoani Lindi kuendelea na mkutano mwingine na kueleza kuwa viongozi wa mkoa huo wana msimamo mmoja, hivyo utafanyika.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Thobias Sedoyeka, alisema walipokea barua kutoka kwa uongozi wa CUF Wilaya ya Mtwara wakiwaomba wazuie mkutano huo.

Sedoyeka alisema taarifa hiyo ya CUF Wilaya ilionyesha kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kutokea katika mkutano huo ndiyo maana wakalazimika kuuzuia.

“Tulilazimika kuzuia mkutano huo na endapo watakaa chini na kupanga taratibu zao vizuri, hatuna tatizo na tutaruhusu kuendelea na taratibu zao. Tumelazimika kuzuia kuhofia uvunjifu wa amani kama barua ya CUF Wilaya ya Mtwara ilivyojieleza,” alisema Sedoyeka.

Naye Mwenyekiti wa JUVICUF Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga mkaani Lindi, Hamidu Bobali, aliwataka wafuasi wa chama hicho kujiongeza baada ya polisi kuzuia mkutano huo kisha waamue kufanya uamuzi sahihi.

Mkutano huo umezuiliwa wakati mwezi uliopita viongozi wa chama hicho Wilaya ya Mtwara walimpokea Profesa Lipumba aliyefanya ziara ya siku mbili mkoani hapa na kufanikiwa kufanya mkutano bila zuio lolote la polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles