22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yatua Bakwata

Mufti Abubakar Zuberi*Wadaiwa kuingiza magari 82 kwa misamaha ya kodi

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RUNGU la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) limeonekana kushika kasi  na safari hii limeangukia kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Kwa mujibu wa barua ya TRA, Bakwata imetakiwa kutoa maelezo ya ongezeko la maombi ya msamaha wa kodi katika utoaji wa magari yanayopitishwa katika taasisi hiyo ya dini, kutoka nje ya nchi.

Hayo yamo katika barua ya TRA ya Novemba 19, mwaka huu  kwenda kwa Katibu Mkuu wa Bakwata yenye kumbukumbu namba MK/TRA/09/VOL.5/107 ya Oktoba 9 mwaka huu iliyokuwa ikitaka punguzo la kodi ya gari aina ya Iveco yenye Chassis namba WJME2NM-4000428502.

Barua hiyo ya TRA inaeleza kwa sababu za kutokubali ombi hilo zimechangiwa na takwimu zinayoonyesha kwamba taasisi hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la maombi ya msamaha ya kodi kwa magari kutoka nje.

Kwa mujibu wa barua hiyo,  tangu mwaka 2006 hadi Septemba  mwaka huu Bakwata imekwisha kuingiza magari 82 ya aina tofauti.

Barua hiyo iliyosainiwa na Meneja Misamaha ya Kosi wa TRA, Mwantum Salim, ilieleza kwamba kutokana na idadi kubwa ya magari ya msamaha pamoja na maombi yanayoongezeka  uamuzi  umechukuliwa wa kufuatilia kwa karibu kujua jinsi magari hayo yanavyotumika katika shughuli za taasisi kabla ya kuendelea kutoa misaada zaidi.

TRA imetoa  siku saba kwa Bakwata iwe imewasilisha   kadi za usajili wa magari, kitabu kinachoonyesha safari za magari, stakabadhi za kulipia mafuta, bima, huduma za matengenezo ya magari ikiwamo  ushahidi wa maelezo na ushahidi kuhusu fedha zilizotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka za taasisi.

“TRA iliitaka Bakwata kuhakikisha inakamilisha hayo yote iweze kushughulikia maombi hayo ya kupata msamaha wa kodi wa gari aina ya Iveco kwa haraka,” ileleza barua hiyo ya TRA kwa Bakwata.

Mufti awa mbogo

Taarifa kutoka ndani ya Bakwata ziliambia MTANZANIA kwamba baada ya barua hiyo ya TRA, Sheikh Mkuu, Mufti Abubakari Zuberi, aliitisha kikao na kujadili suala hilo kati yake na Katibu Mkuu wake, Suleiman Lolila  kuweza kupata maelezo ya kina.

“Katika kikao cha Mufti Zuberi, Katibu Mkuu Lolila, alitakiwa kutoa maelezo ya jambo hili lakini naye aliruka na kusema hausiki nalo ila linamhusu Naibu Katibu Majaliwa.

“Tangu baada ya kuletwa   barua hii hapa, Bakwata kumekuwa hakukaliki hasa kwa watendaji wa juu akiwamo Katibu Mkuu na inaonekana Mufti Zuberi hana mchezo wa hili suala.

“Tena ni wazi haya yamekuwa yakifanyika kwa kipindi kirefu sana,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Bakwata.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Bakwata, Suleiman Lolila,  kupata ufafanuzi wa barua hiyo ya TRA, simu yake haikupokelewa licha ya kupigwa kwa zaidi ya mara saba kwa vile   simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Mwandishi wa habari hii alimtumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu, Katibu Mkuu huyo wa Bakwata  lakini nao hakuujibu hadi tulipokuwa tunakwenda mitamboni jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles