Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WENYEVITI wa Mikoa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamempongeza kwa dhati Rais Dk. John Magufuli kwa kasi ya utendaji wake.
Kwa mujibu wa wenyeviti hao, kasi ya Rais Magufuli hasa ya kuwachukulia hatua watendaji wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ni kazi inayokwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Pongezi hizo zimetolewa Mwenyekiti wa Wanyeviti wa Mikoa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ramadhani Madabida alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Madabida ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar es Salaam, alisema wenyeviti wanampongeza Rais kwa dhati kutokana na hatua zinazochukuliwa dhidi ya watendaji hao wa Serikali.
Alisema watendaji hao wa Serikali walikuwa wakifanya kazi na hata kutoa huduma isiyo bora kwa wananchi, hivyo kila mtu kwa nafasi yake afanye kazi kwa mujibu wa sheria.
“Kwa kasi hii ya Dk. Magufuli sisi wenyeviti wa CCM wa mikoa tunamuunga mkono na tupo tayari kwa uamuzi wowote atakaochukua hata kwa viongozi wa CCM ambao pia nao wamekuwa hawafuati utaratibu.
“Tunawaomba Watanzania waendelee kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Magufuli ikiwamo ya kuhakikisha kila mtu anawajibika katika nafasi yake ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Madabida.