30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: Rais Magufuli ametupa rungu

4NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema kuanzia sasa inaanza kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuwakamata wafanyabiashara watakaokwepa kulipa kodi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, alisema uamuzi wa kuwakamata wafanyabiashara ambao siku za nyuma walikuwa wakikingiwa kifua na watendaji wa Serikali, utaanza mara moja baada ya kupata baraka za Rais Magufuli wiki iliyopita.

Alisema katika kikao chao na Rais Magufuli, aliwataka kuziba mianya ya wakwepa kodi na kuwaweka hadharani mbele ya jamii ili wajulikane, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kuhusu makusanyo, Bade alisema mwaka 2015/16, agizo la Serikali liliwataka wakusanye Sh trilioni 12.3 kwa mwaka ambazo kutokana na mwenendo mzuri wanatarajia kuvuka lengo.

Alisema hadi sasa, makusanyo yameongezeka kwa asilimia 17, baada ya kufanikiwa kukusanya Sh trilioni 3.778 Julai hadi Oktoba kiasi ambacho ni sawa na asilimia 97.6.

Bade alisema Julai, mwaka huu, TRA ilikusanya sh bilioni 849,582.9 ambazo ni sawa na asilimia 99.4, wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh bilioni 854,922.9.

Alisema Agosti, walivuka lengo kwa kukusanya Sh bilioni 890,536.7 sawa na asilimia 101.5, wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh bilioni 876,974.2.

Bade alisema Septemba walikusanya Sh trilioni 1,067,888.3 sawa na asilimia 91.7, huku lengo likiwa ni kukusanya Sh trilioni 1,163,999.4 na Oktoba walikusanya Sh bilioni 970,089.6 sawa na asilimia 99.3, wakati lengo lilikuwa  kukusanya Sh bilioni 976,441.5.

“Kutokana na makusanyo hayo, mwenendo wa makusanyo kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 17 na tunaona jinsi gani unakaribia kufikia lengo, hasa ikizingatiwa Rais Magufuli ameweka msisitizo wa kazi, hivyo natumai tutavuka lengo,” alisema Bade.

Alisema mafanikio hayo yametokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na mamlaka, ambayo inamtaka kila mfanyakazi kuwajibika ipasavyo.

Bade alisema wanaamini mwaka huu watavuka lengo kutokana na msisitizo wa Rais Magufuli wa kukusanya mapato bila woga wala kumwonea mtu.

Aliwataka wafanyabiashara na wadau wote wa kodi kutimiza wajibu wao wa kulipa kwa hiari ili kuchangia pato la taifa.

“Katika kuhakikisha tunafanikisha lengo letu, suala la ukusanyaji wa mapato tunatarajia kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara ili tuone changamoto tuliyopewa ya kukusanya zaidi ya kile tunachokitarajia mwaka huu, tunatimizaje,” alisema Bade.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles