23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli kuiona Stars, Algeria

DSC_0277*Mecky Sadiki amwalika Kikwete

*Algeria yapata pigo jingine

THERESIA GASPER NA BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi kati ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ dhidi ya Algeria ‘The Desert Foxes’, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kuhudhuriwa na Rais huyo mpya tangu kuapishwa kwake Novemba 5 mwaka huu, huku Algeria wenyewe wakitarajiwa kuingia nchini leo.

Akizungumza jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema ujio wa Rais uwanjani utasaidia kuhamasisha wachezaji kufanya vizuri na kupata mabao mengi katika mchezo huo.

“Kwa asilimia kubwa tunatarajia Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi, labda itokee dharura tunawaomba wana Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi ili kuleta hamasa, ulinzi katika mchezo huo umeimarishwa hivyo watu wasiwe na wasiwasi wajitokeze lakini mashabiki ambao wamekuwa wakileta ushabiki wa timu zao waondoe hali hiyo badala yake wawe kitu kimoja na kushangilia timu ya Taifa,” alisema.

Sadiki aliongeza kuwa amemwalika Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete kuhudhuria mchezo huo ili kuleta hamasa zaidi kwa kuwa ni mmoja wa watu ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya michezo.

Katika hatua nyingine wadhamini wamezidi kujitokeza kuisaidia Stars, ambapo Mfuko wa Pensheni wa PPF, umetoa kiasi cha shilingi milioni 5, huku Jubilee Insurance ikikabadhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuisapoti Taifa Stars.

Juzi timu hiyo ilipata udhamini kutoka katika Hoteli ya Serena wa kiasi cha shilingi milioni 20 pamoja na Benki ya Equity ambayo ilitoa kiasi cha Dola za Marekani 10,000 (zaidi ya shilingi milioni 22 za Tanzania) ikiwa ni mchango wa kuisaidia timu hiyo.

Wakati huo huo Algeria ‘The Desert Foxes’ wamepata pigo jingine baada ya nyota wao, Yassine Brahimi, kuumia katika mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mchezo wa Jumamosi dhidi ya Taifa Stars.

Chama cha Soka nchini Algeria (FAF), kimesema Brahimi anayekipiga katika klabu ya FC Porto ya Ureno ataukosa mchezo wa awali dhidi ya Stars baada ya kupata majeraha wakati wa mazoezi ya mwisho kabla ya kuanza safari ya kuja nchini.

Hata hivyo, chama hicho kimesema mshambuliaji huyo anaendelea na matibabu lakini bado haijajulikana atachukua muda gani kuendelea kupata matibabu.

Nyota huyo wa FC Porto, amekuwa na mchango mkubwa wa kuisaidia timu hiyo katika michuano mbalimbali akisaidiana na mastaa wenzake ambao wanakipiga katika klabu mbalimbali barani Ulaya kama vile Ryad Mahrez anayechezea klabu ya Leicester City nchini England.

Nyota mwingine ambaye Algeria watamkosa ni kiungo mshambuliaji, Sofiane Feghouli, anayekipiga katika klabu ya Valencia ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini Hispania ikishika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi.

Wakati huo huo, Stars iliwasili nchini jana ikitokea Afrika Kusini ambako iliweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo huku wachezaji wake wakiendelea vema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles