24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tozo masoko ya samaki kimataifa kuwasilishwa wizarani

Na Mwandishi Wetu, Geita

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wakurugenzi wa halmashauri zenye masoko ya samaki ya kimataifa kuacha kupanga tozo za mazao ya uvuvi bila kuwasiliana na wizara ili kuondoa kero zinazowakumba wafanyabiashara katika maeneo hayo.

Akizungumza jana Januari 3, mara baada ya kutembelea mnada wa mifugo uliopo Kijiji cha Buzirayombo Kata ya Bukome na soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato mkoani Geita, Waziri Ndaki amesema wizara haitaki kusikia kero za wafanyabiashara kuhusu tozo zisizo rafiki katika masoko hayo likiwemo soko la samaki la kimataifa la Kata ya Kirumba lililopo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk. Medard Kalemani (wa kwanza kulia) pamoja na viongozi wengine wa serikali wakati akikagua shughuli mbalimbali zinazoendelea katika soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

“Wakurugenzi walio na masoko haya ya kimataifa kwa maana ya soko la Kirumba na Kasenda, sisi wizara hatutaki kusikia kelele, mnapopanga tozo zenu hakikisheni kwa masoko haya mawili tuwasiliane ili tupange tozo ambazo zitakuwa rafiki,” amesema Ndaki

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk. Medard Kalemani, amemuomba Waziri Ndaki kupitia vikundi vya wavuvi vilivyosajiliwa, wizara ione namna ya kuwasaidia mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuwanunulia nyavu ili kuacha kujihusisha na uvuvi usiofuata utaratibu.

Nao baadhi ya wavuvi na wananchi wanaofanya shughuli za kibiashara katika soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda wamesema wanashirikiana na serikali kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Soko la Samaki la Kimataifa, Suleiman Said (wa pili kushoto) mara baada ya kutembelea soko hilo lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Aidha wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi namna inavyofanya jitihada za kuhakikisha inaboresha mazingira ya wavuvi ili sekta hiyo iweze kuwa na tija kwa wadau na hatimaye waweze kunufaika kiuchumi.

Waziri Ndaki pia amekagua ujenzi wa machinjio ya kisasa yanayojengwa katika eneo la mnada wa mifugo Kijiji cha Buzirayombo Kata ya Bukome, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles