33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mlundikano wa uchafu Bariadi wapata suruhisho

Na Derick Milton, Bariadi

Wakazi wa mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, sasa wataondokana na changamoto iliyodumu kwa muda mrefu ya mlundikano wa uchafu kwenye maeneo ya kukusanyia taka katikati ya mji huo baada ya halmashauri hiyo kuleta vifaa vipya vitakavyotumika kukusanya taka kwa haraka na kwa wakati.

Mji huo umekuwa na changamoto kubwa ya uwepo wa uchafu ambao umekuwa ukilundikwa kwenye maeneo ya kukusanyia taka na kukaa muda mrefu bila ya kusombwa hali ambayo ilikuwa ikihatarisha uwepo wa magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu.

Wafanyabiashara wengi wakubwa, wadogo, na wa kati katika soko kuu la Bariadi, wamekuwa wakilamika kutosombwa uchafu kwenye soko hilo licha ya kutozwa ushuru wa uchafu kila mwezi, ambapo wengi wao walikuwa wakidai kuwa uchafu ulikuwa ukihatarisha Afya zao kutokana na harufu kali.

Akiongea na MtanzaniaDigital leo Januari 4, mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkurugenzi wa halmashuari hiyo, Merkzedeck Humbe amesema kuwa vifaa hivyo vipya vimegharimu zaidi ya Bilioni moja kupitia mradi wa kuendeleza miji (USDP).

Humbe amesema kuwa vifaa hivyo ni pamoja na Gari moja kubwa la taka ngumu, Gari la moja la maji taka pamoja kijiko cha kuzolea taka ambapo amesema kuletwa kwa vifaa hivyo itaondoa changamoto ya mji huo kuwa mchafu.

“Mji wetu umekuwa ukizalisha taka nyingi kuliko uwezo ambao tulikuwa nao kuzoa, hatukuwa na vifaa vya kutosha na bora, tulilazimika kukodi kutoka Mwanza na gharama zilikuwa kubwa na zilikuwa zinatushinda,” amesema Humbe.

Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu, Pitter Subadi, amesema kuwa uzalishaji wa taka katika mji huo ni tani 30 kwa siku, ambapo kabla ya kuletwa kwa vifaa hivyo walikuwa na uwezo wa kusomba tani 10 peke yake.

“Kwa vifaa hivi sasa tutakuwa na uwezo wa kusomba tani 25 kwa siku kati ya 30 zinazozalishwa, kilichobaki ni kontena za kuweka kwenye maeneo ya kukusanyia taka, zikifika hizo tutakuwa na uwezo wa kusomba taka zote kwa wakati mmoja na haraka,” amesema Subadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles