Aveline Kitomary, Dar es salaam
UBORESHAJI na utoaji huduma bora za afya ni sehemu muhimu katika ustawi wa maendeleo ya jamii.
Afya bora huambatana na maendeleo ya kiuchumi,kijamii na hata kielimu.
Hivyo basi upatikanaji wa huduma bora za afya huchochea maendeleo katika nchi yoyote ile ambayo inatarajia kupiga hatua katika uchumi.
Serikali imejitahidi kwa kiasi chake kuendelea kuboresha huduma za afya katika vituo vya afya na pia kwa upande wa huduma za kibingwa .
Hivi sasa huduma za kibingwa kama matibabu ya juu ya saratani,moyo, figo, ubongo,mishipa ya fahamu na mengine yanapatikana ndani ya nchi.
Hatua hii imefanya wagonjwa wengi kupata matibabu ndani ya nchi kuliko kupewa rufaa kwenda kupata matibabu nje ya nchi jambo ambalo limeokoa gharama nyingi.
Tiba Mtandao ni huduma za afya zinazotolewa kwa kutumia njia ya Tehama ambapo picha za X-ray huweza kutumwa kutoka hospitali moja kwenda nyingine na kuangaliwa na mtaalmu wa afya na majibu kurudishwa katika hospitali husika.
Matumizi ya mfumo huo umekuwa ukishamiri zaidi katika nchi zilizoendelea na umeweza kurahisisha huduma za matibabu za kibingwa na kawaida kutoka hospitali ndogo kwenda hospitali kubwa.
Matunda ya huduma hizo yameweza kuonekana katika nchi zilizoendelea baada ya kurahisishwa kwa huduma za matibabu hadi ngazi ya zahanati hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa corona.
Hapa nchini Novemba 14 mwaka jana Serikali ilizindua mpango wa kuanzisha huduma za tiba mtandao nchini.
Akizindua mpango huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema lengo la tiba mtandao ni kurahisisha huduma za kibingwa kuwafikia wananchi kwa kiwango kikubwa.
Baada ya hatua hiyo Juni 19 mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ilizindua rasmi kituo cha matibabu cha kitaifa cha tiba mtandao kilichopo katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ambapo tayari hospitali ya Mkoa wa Morogoro imeunganishwa na huduma hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema kuwa huduma hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
“Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli imefanya mambo makubwa katika ngazi za afya ya msingi, zahanati na bajeti za zimeongezwa dawa.
“Kwa mwaka 2015 wakati inaingia madarakani kulikuwa na nyumba sita vya kufanya upasuaji hapa MOI na leo kuna vyumba tisa hii imepunguza muda wa mgonjwa kufanyiwa upasuaji awali watu walikuwa wakipewa huduma hiyo wiki sita lakini sasa hata wiki moja haiishi anaweza kupata huduma.
“Kabla ya hapo vitanda vya ICU vilikuwa nane sasa tunaweza kulaza watu 16 na pia HDU ilikuwa hamna lakini sasa kuna vitanda vinane kwa MOI tumetumia bilioni 17.9 kwajili ya kununua vifaa tiba tumeweka CT- scan za kisasa, MRI,Ventilator na vifaa vingine,”anabainisha Ummy.
Waziri Ummy anasema kutokana na huduma za afya kuboreshwa rufaa za nje zimepungua ambapo kabla ya mwaka 2015 asilimia 20 kati ya wagonjwa 100 waliokuwa wanahitaji upasuaji wa mifupa walipelekwa nje ya nchi.
Anasema idadi hiyo imepungua ambapo kwa sasa katika kila wagonjwa 100 wanaopelekwa nje ni wawili.
“Lakini wagonjwa ambao wanahitaji upasuaji wa mishipa ya fahamu katika kila wagonjwa 100 walikuwa wanapelekwa nje wagonjwa 40 na sasa wamepungua hadi watano hata Mtanzania masikini sasa anayehitaji huduma ya mifupa na upasuaji mishipa anaweza akapata ndani ya nchi.
Waziri Ummy anasema kutokana na kuendelea kuboreshwa kwa huduma katika sehemu mbalimbali nchini yamechangia urahisi wa matumizi ya tehama ikiwemo tiba mtandao .
“Kwa maeneo mengine tumeweza kuboresha huduma nafurahi leo tumeweka alama katika matumizi ya tehama katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini naamini tunaweza zaidi, niwapongeze taasisi ambayo imekuja na mradi huu na kutekelezwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na ofisi ya Rais Tamisemi.
“Mradi huu utawezesha kuunganisha hospitali ngazi ya Wilaya, hospitali za halmashauri pamoja na hospitali za rufaa za mikoa na Hospitali za taifa,”anaeleza.
FAIDA ZA TIBA MTANDAO
Waziri Ummy anasema mradi huo wa tiba mtandao utaondoa kero na ugumu wa wananchi kupata huduma za kibingwa na kupunguza gharama za matibabu
“Utapunguza gharama za usafiri kutoka mikoani kuja MOI, Muhimbili au Hospitali za rufaa za kanda kama Mbeya, KCMC na Bugando hata huduma za malazi zitakuwa hazipo.
“Mradi huu ni muhimu sana hilo nasisitiza kuwa tunatakiwa kwenda kwa kasi katika kusambaza huduma hii ya tehama kwenye hospitali zingine kwani ukikamilika utawezesha kuunganisha hospitali za kanda za rufaa na za wilaya 15 na kituo cha MOI lakini pia itawezesha huduma za picha X-ray,”anaeleza.
Anabainisha kuwa katika miaka ijayo huduma ya tiba mtandao itakuwa sehemu ya huduma inayotewa na bima ya afya(NHIF).
Ummy anasema tiba mtandao itarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za afya kwa haraka bila kujali eneo mwananchi alipo
“Faida zingine ni kuongeza uzoefu kwa wataalamu wa afya kutoka kwa wataalamu wabobezi ambao watakuwa wakiwasiliana nao hii itaboresha utoaji wa huduma.
“Pia itasaidia kuboresha utambuzi wa magonjwa kwa haraka na ufanisi kwa kuwa wataalamu wabobezi watakuwa wakihudumia wananchi wengi zaidi hata walioko mbali na hospitali wanazotolewa huduma,”anasema
MFUMO WA RUFAA KUZINGATIWA
Mfumo huo wa tiba mtandao unatajwa kupunguza rufaa ambazo sio za lazima kutokana na wananchi kuhudumiwa katika hospitali walizopo
Hivyo Ummy alitoa wito kwa taasisi za umma ambazo imeungana na Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba wanaongeza idadi ya hospitali zinazounganishwa na mradi huu.
“Ni vyema katika mfumo huu rufaa ikazingatiwa, vituo vya afya vikaunganishwa na hospitali za Wilaya na hospitali za wilaya zikaunganishwa na hospitali za mkoa za Rufaa na rufaa kuletewa moja kwa moja kwenye kituo cha MOI.
“Kwamba vituo vya afya vitume kwa ngazi za hospitali za rufaa ya mkoa ambapo kuna mashine za CT -scan lakini kwa hospitali za kanda tutaweka MRI.
“Kwa mfumo huu wa rufaa ningetamani tuunganishe hospitali zote za rufaa 28 za serikali, tuunganishe hospitali zote za halmashauri za serikali takribani 145 lakini pia vituo vya afya ambao kuna watu wengi wenye changamoto .
Anasema wataendelea kuunganisha mfumo huo kwa hospitali zingine hadi watakapofikia zote za umma na binafsi ambazo hazina wataalamu wabobezi.
WATAALAMU KUONGEZWA
Waziri Ummy anasema upatikanaji wa wataalamu ambao wanatoa huduma za tiba mtandao(radiologist) ni changamoto kwasasa kutokana na kuzalisha wa wataalamu wachache katika vyuo.
“Kwa chuo cha MUHAS wataalamu walikuwa wanazalishwa chini ya 10 lakini sasa hivi wanazalisha 20 kwa darasa lililopo, nikiangalia takwimu tuna hospitali za kitaifa sita,za rufaa za kanda sita, hospitali za rufaa za mikoa 36, hospitali za wilaya 331.
“Na tangu mwaka jana tumefaulu kuweka X-ray, hadi vituo vya afya tumeruhusu kuweka X-ray na Ultrasound kwa mwaka huu vituo 480 vimejengwa kwahiyo ni vyema tukajitahidi tukawa na wataalamu wa kutosha kwa sababu tunaendelea kupanua huduma hizi.
“Sasa katika hospitali ya Wilaya na Rufaa ya Mkoa tutawajibika kuwa na wataalamu watakaochukua picha na kuzituma MOI na wataalamu wa kusoma picha ya mionzi watazisoma na kurudisha majibu papo kwa hapo hivyo tunatakiwa tuwe na wataalamu wa kutosha,”anabainisha Ummy.
HUDUMA NJE YA NCHI
Waziri Ummy anaeleza kuwa pia wana malengo ya huduma hiyo kuunganishwa nje ya nchi hasa nchi za jirani ili kupanua wigo zaidi.
Licha ya malengo hayo anasema mpango mwingine ni kuunganisha huduma ya hiyo na huduma maalum za kibingwa.
“Lakini pia ni vyema tukafikiria kupanua zaidi huduma hii hadi nje ya nchi ni jambo jema zikifika hata Comoro,Uganda ,Burudi na Kenya itasaidia kupanua wigo wa matibabu kwa mataifa ya nje.
“Ni matarajio yangu tutaanzisha kituo kama hiki kwenye kanda na hospitali ambazo zinatoa huduma maalum kama huduma za moyo zitatolewa kupitia tiba mtandao ,huduma za mionzi kwa ajili ya ugonjwa wa saratani na zingine,”anafafanua.
Anasema kuwa Wizara ya Afya itakamilisha mwongozo wa matumizi ya tiba mtandao ili kusaidia kusimamia kwa ukamilifu matumizi sahihi ya huduma hii bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa ukizingatia haki ya faragha.
Anasema kwa mwaka huu hadi kufikia mwezi Oktoba wanataraijia kuunganisha hospitali 10 .
“Natoa maelekezo kwa hospitali za umma kuweza kuunganishwa na tiba mtandao tutaacha X-ray za zamani na tunataka za kisasa hata wadau wakitoa mzikatae tusiwe tunapokea kila kitu,”anasisitiza.