Asha Bani, Dar es Salaam
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umelaani wananchi kuwashambulia na kuwaua askari watatu wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mratibu wa mtandao huo, Deogratias Bwire, imeeleza kitendo hicho ni cha kikatili dhidi ya Polisi.
“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, polisi watatu akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nguruka (Ramadhani Mdimi), Uvinza mkoani Kigoma walishambuliwa vibaya na wananchi waliokuwa na silaha za jadi na kusababisha vifo vya askari hao,” imesema taarifa hiyo.
Amesema THRDC inafanya kazi kama mwamvuli wa watetezi wa haki za binadamu nchini imekuwa mstari wa mbele katika kutambua na kutetea haki za Watetezi wa Haki za Binadamu wakiwamo polisi.
Pamoja na mambo mengine, amesema jitihada zimekua zikifanywa na THRDC katika kutambua, kuwatetea na kuwalinda askari wetu wanaofanya kazi kubwa ya kuwalinda raia na mali zao.
“Mtandao unapenda kutoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Siro, Jeshi la Polisi kwa ujumla, ndugu wa marehemu na Watanzania wote kwa kupoteza nguvu kazi ya taifa,” amesema.