32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TETEMEKO LA ARDHI LAUA POLISI

Na WAANDISHI WETU-MWANZA/BUKOBA


TETEMEKO la ardhi lililotokea katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera, limesababisha kifo cha askari WP Koplo Joyce Jackson wa Kituo cha Polisi Misungwi.

Mbali ya kifo hicho, pia limejeruhi watu watatu wakiwamo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.

 Tetemeko hilo lililotokea jana saa 6:55 mchana na kudumu kwa muda wa dakika moja, limesababisha taharuki kubwa katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kwa baadhi ya wananchi wa mikoa ya Mwanza na Kagera ambao walilazimika kukimbilia ofisi zao kwa hofu ya kuangukiwa na majengo.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema walikuwa  wamepumzika nje ya Kituo cha Polisi Misungwi,  baada ya kutokea tetemeko la ardhi na Koplo Joyce alidondoka chini na kupoteza fahamu.

Alisema walimsaidia kumkimbiza hospitali, lakini wakati wanamfikisha alikuwa tayari amefariki dunia.

“Joyce alianza kazi jana, baada ya kumaliza likizo ya uzazi. Alijifungua kwa njia ya upasuaji na ameacha kichanga, alikuwa pia  anasumbuliwa na shinikizo la damu (presha),” alisema shuhuda huyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Dk. Marcelina Kiemi, alithibitisha kupokea mwili wa Koplo Joyce na majeruhi ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.

“Baada ya kutokea tetemeko la ardhi, nimepokea mwili wa askari polisi wa kike Joyce Jackson ambaye alikuwa tayari amefariki dunia,” alisema Kiemi.

Dk. Kiemi, alisema majeruhi watatu; Anna Habi (18) mwanafunzi wa kidato cha nne, Mathayo Ndalahwa (15) kidato cha kwanza kutoka Shule ya Sekondari ya Igokelo na mahabusu Mathias Simoni (22) mkazi wa Kijima, wamelazwa na wote hali zao zinaendelea vizuri.

 Mwalimu wa Shule ya Sekondari Igokelo, Adela Sakoma, alisema wakati tetemeko hilo linatokea walikuwa darasani, ndipo wanafunzi walianza kukimbizana kutoka nje kupitia mlangoni ili kunusuru maisha yao.

Alisema baadhi yao walijeruhiwa na kuwakimbizwa hospitalini.

 

RPC MSANGI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kifo cha Koplo Joyce.

Alisema kwa muda sasa, Koplo Joyce alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha.

“Huyu WP Koplo Joyce alikuwa na tatizo la presha, wakati tetemeko linatokea wakiwa wanatoka nje, alianguka ghafla. Wenzake walimsaidia na kumkimbiza hospitalini na walipomfikisha tayari alikuwa amepoteza uhai,” alisema Kamanda Msangi.

 

ILEMELA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga, Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Leonard Masale, baadhi ya wakuu wa idara na wadau wengine waliokuwa na kikao kwenye ofisi za manispaa hiyo, walilazimika kutimua mbio wakihofia kuangukiwa na ukuta.

Meya wa Manispaa hiyo, Renatus Mulunga, watumishi wengine wa halmashauri, wananchi waliokuwa wakipata huduma mbalimbali na watumishi wa tawi la Benki ya NMB lililopo eneo hilo, nao walitimua mbio kujinusuru.

Wafanyabiashara katika la soko la machinga na wakazi wa maeneo jirani na majengo ya halmashauri hiyo, walionekana wakitoka nje huku wakipiga mayowe wakati tetemeko hilo lilipopita maeneo ya Buswelu.

 

BUKOBA

Wilayani Bukoba mkoani Kagera, wananchi waliozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, walisema waliingiwa na hofu na kupata taharuki kubwa baada ya kusikia tetemeko hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Juliana Rubeja, alisema tetemeko hilo lilitokea wakati akiwa katika biashara yake ya kuuza ndizi ambapo alisikia mtikisiko uliodumu kwa muda wa dakika moja.

“Niliposikia kwa kweli nilishtuka, jambo la  kwanza nililolifikiria ni watoto wangu. Nilizazimika kukimbilia nyumbani kwenda kuwaangalia, nashukuru Mungu amesaidia hakuna baya lolote lililotokea,” alisema Rubeja.

 Musa Issa, alisema alikuwa katika kazi yake ya ushonaji na akaona kiti alichokuwa amekakalia kinatikisika, akainuka na kusogea pembeni ili kuona kinachoendelea na hali ilivyotulia alirudi na kuendelea na kazi.

“Jamani mimi sikuelewa ni nini kimepita, sijaelewa. Hali hii itatokea hivi mpaka lini jamani au ndio siku za mwisho hizi!” alisema Issa kwa mshangao.

Kwa mujibu wa wataalamu wa jiolojia, tetemeko la ardhi husababishwa na kuvunjika au kugongana kwa miamba iliyoko sehemu zenye kina kikubwa chini ya ardhi kutokana na nishati kubwa iliyojilimbikiza kwa muda mrefu kutoka ghafla hivyo husababisha kutetemeka kwa ardhi.

 

Uchunguzi na ufuatiliaji wa muda mrefu umethibitisha kuwa tetemeko la ardhi hutokea sehemu yenye kina cha zaidi ya kilomita 10 hivi chini ya ardhi, hivyo ni hali ya kimaumbile inayotokea mara kwa mara duniani takriban kila siku, lakini asilimia kubwa ya matetemeko hayasikiki na yapo yanayosikika wakati yakiwa na nguvu ya kiwango fulani cha juu au chini.

Tetemeko hilo ni la tatu kutokea, baada ya lile la Septemba 10, 2016 lililokuwa na nguvu ya 5.7 katika vipimo vya richter na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi, huku nyumba zaidi ya 200 zikibomoka.

 

Habari hii imeandaliwa na TWALAD SALUM,  PETER FABIAN, JUDITH NYANGE (MWANZA) NA RENATHA KIPAKA (BUKOBA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles