ADAM MKWEPU NA MITANDAO
BINADAMU huishi mara moja tu katika ulimwengu huu ambao hesabu za muda wa kuishi hufananishwa na maisha ya umeme wa luku ambao huishi muda mrefu kutokana na  matumizi ya mhusika.
Tabia moja ya umeme wa luku ambayo watu wengi hawaipendi ni ile ya kuzimika kwa umeme ghafla bila ya kuzingatia upo sehemu gani au upo na nani.
Luku haina muda wa kukusubiri au kukuhurumia, badala yake hufanya kile ambacho ni sahihi kwa wakati huo kutokana na utaratibu wake.
Hivyo ndivyo ilivyo hata katika maisha ya ulimwengu wa soka, muda ukifika hakuna kukuhurumia eti umeanza kuwa katika ubora wako, jambo hilo halipo katika soka.
Miaka ya nyuma wakati Ronaldo de Lima akitangaza kustaafu soka alilia kwa uchungu kwa kuwa luku ilikwisha, huku ikimkuta eneo nyeti katika utamaduni wa wapenda soka duniani.
Ronaldo alihitaji muda urudi nyuma ili aendelee kuishi maisha aliyozoea akiwa uwanjani, kitu ambacho kilitofautiana na utaratibu wa umeme wa luku.
Nyota wa West Ham, Dimitry Payet amekuja kuonekana  katika ulimwengu wa soka  la wachezaji wenye kiwango bora ulimwengu tayari jua limeshazama,  hivyo hana wa kumlaumu luku ikikata.
Sainti Carzola wa Arsenal kila akitazama saa yake na kalenda sidhani kama anafurahia kushuhudia kasi yake huku msimu ukimalizika akiwa hana kitu alichofanya uwanjani zaidi ya kupata majeraha yatakayomfanya kukaa nje ya uwanja miezi mitatu.
Nyota huyo kwa sasa ana umri wa miaka 31, ambapo kwa utamaduni wa umeme wa luku ikifika katika mishale hiyo haishangazi kuona kinachoendelea kutokea kwake.
Nani hakupenda kuendelea kumuona beki wa Chelsea, John Terry uwanjani kwa sasa ambapo timu hiyo inaongoza Ligi Kuu England?
Ikiwa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England na timu ya Real Madrid, Fabio Capello, anatamani maisha yarudi nyuma aendelee kuwa na beki huyo nani wa kupinga?
Capello aliwahi kuulizwa na shabiki wa soka England, kwanini alikuwa akimpanga Terry katika kikosi cha timu ya taifa hata akiwa katika kiwango kibovu.
Jibu lake likawa rahisi tu kwamba ni mchezaji mwepesi na mwenye kuyajua majukumu yake ipasavyo akiwa ndani ya uwanja.
Capello akiwa ndani ya vyumba vya kubadili nguo mara kadhaa humkuta Terry ndio mchezaji pekee wa England ambaye hakati tamaa  mapema, badala yake hutumia muda huo kuwaleta wenzake pamoja.
Terry hakuwa mwoga wa kupambana na kuwafanya wenzake kuondoa woga wakiwa uwanjani.
Ni mara ya kwanza katika maisha ya mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich kushuhudia Terry akiwa nje ya uwanja katika mchezo mkubwa kama wa Tottenham au Manchester City, ni jambo geni lakini la kawaida kama umeme wa luku ukiwa umekwisha.
Majeraha ndiyo yanayomwangusha Terry, huku kocha wake, Antonio Conte akipanga kumvua unahodha kipenzi hicho kwa mashabiki wa Stamford Bridge.
Huenda Terry akawa haamini kinachotokea miguuni mwake, lakini huo ndio  ukweli mchungu na  tayari wanaojua utaratibu wa umeme wa luku wameanza kumhusisha na kujiunga na timu ya China ya Shanghai Shenhua katika usajili wa dirisha dogo la Januari mwakani, ili akamalize kila kitu huko.
Wakati ni ukuta ukifika hakuna wa kuzuia hata kama ukilia vipi, nani anajua uchungu wa Terry kushindwa kutema cheche zake uwanjani huku ukizingatia timu yake ilikuwa ikicheza dhidi ya Manchester City au Tottenham?
Lakini hilo haliwezekani tena kwa sasa akitarajia kutimiza umri wa miaka 36 wiki hii, hata hivyo, bado atakumbukwa na wapenda soka duniani, ingawa miguu yake haiwezi kujibu maswali magumu anayojiuliza.
Miaka 18 aliyotumia uwanjani hadi sasa ina ushuhuda wa kile anachotaka kiendelee, licha ya kuwapo kwa ugumu wa kutokea kwa sasa.
Terry alikuwa mchezaji mwenye ushawishi mkubwa mwaka 2012 wakati timu yake ikifanikiwa kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Mingwa Ulaya dhidi ya  Bayern Munich.
Beki huyo pia ameifanya dunia kushuhudia vingi vya kupendeza uwanjani na vile vya kuchefua, wakati mwingine kuudhi kutokana na matukio mbalimbali, lakini iliburudika kupitia kwake pale alipoweza kuzisimamisha nywele za mashabiki wake kwa furaha.
Hadithi  nzuri ya Terry na Chelsea ilianza tangu mwaka 2004 ambapo alitangazwa kuwa nahodha wa timu hiyo akiwa chini ya utawala mpya wa kocha Jose Mourinho, baada ya kuondoka kwa Claudio Renieri.
Simulizi hiyo hadi sasa haiwezi kutoka katika vichwa vya wapenzi wa soka na klabu hiyo kirahisi, hata wakiendelea kufanikiwa kuchukua makombe bila beki huyo.
Ni mchezaji pekee ambaye amekuwa na asilimia 64 ya mafanikio ya klabu hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 1905 ikitokea uwanja wa Fulham Road kabla ya kutengana.
Kwa sasa uamuzi uliobakia ni kwa Conte kuamua tu, kwani msimu uliopita Terry alisababisha faulo 13 na kupokonya mpira mara moja tu msimu mzima.
Mwaka 2011 Terry  alikuwa akitajwa kama mtoaji pasi bora Ulaya na kuonekana aliyefikia malengo ya soka zaidi ya wengine.