20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE APINGA AMRI YA RC MAKONDA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


mwita-waitaraMBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) amepinga amri iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya wafanyabiashara kufunga maduka yao kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa nne ili wafanye usafi.

Amesema amri hiyo ni batili na haitekelezeki kwa sababu inarudisha nyuma uchumi wa wananchi hususani wafanyabiashara ndogondogo ambao wanategemea kipato chao cha siku kuendesha maisha yao.

Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kivule mwishoni mwa wiki, Waitara alisema yeye hapingani na watu kufanya usafi katika maeneo yao, lakini amri ya kufunga maduka kila Jumamosi inaathiri uchumi wa wananchi hivyo ni batili na haipaswi kuendelea kuwapo.

Siku chache baada ya kuteuliwa kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda alipiga marufuku kufungua maduka na biashara zingine kabla ya saa nne asubuhi ili muda huo utumike kufanya usafi na anayekaidi agizo hilo hutozwa faini isiyopungua Sh 50,000.

Mbunge huyo wa Ukonga alisema uchumi wa watu masikini hususan wa mjini unategemea kile wanachokizalisha kila siku, hivyo amri ya kufunga biashara kila wiki ni kurudisha nyuma juhudi za wananchi kujiletea maendeleo yao.

Katika mkutano huo aliwaambia wananchi hao kujiwekea utaratibu kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi wakati wote na kila Jumamosi wafungue biashara zao asubuhi kama kawaida na wasibughudhiwe na mtu yeyote.

“Mimi naunga mkono utaratibu wa kufanya usafi kila mwezi uliotangazwa na Rais Dk. John Magufuli ambao upo kwa mujibu wa taratibu, lakini huu wa kila Jumamosi mimi sina mwongozo nao na hizo faini za kila wiki sizitambui na ni batili.

“Ninachotaka kila mtu afanye usafi kwenye eneo lake, hizi faini zinatozwa bila utaratibu hata kama eneo la mtu ni safi sitaki kuzisikia, wananchi hawa si wanyama, waelimishwe waachwe wajiwekee utaraibu wao.

“Hivi mama, baba ntilie anayepika  maandazi, vitumbua, chapati afunge biashara tangu asubuhi mpaka saa nne halafu hiyo chai itanywewa na nani, huyu mtu unamwambia afunge biashara ili akaibe mtaani?” alihoji mbunge huyo na kuongeza:

“Watendaji lazima muwasikilize watu, nasikia kinachofanyika ni mwendo wa kuviziana, waacheni watu wafanye kazi, hapa ni kazi tu sio faini tu” alisema Waitara.

Katika hatua nyingine, Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule alivunja kikundi cha ulinzi kilichokuwa katika ofisi hiyo kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na kuwanyanaysa wananchi.

Badala yake, alisema uitishwe mkutano wa hadhara watu wote wanaohitaji kazi hiyo walete maombi katika ofisi hiyo na baadaye wajadiliwe na wananchi katika mkutano wa hadhara ili kuepuka kuwapa kazi watu wasiokuwa waaminifu katika jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles