Na Ramadhan Hassan, Dodoma
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemkabidhi Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji Taarifa ya Uboreshaji wa Sheria za Habari zilizoandaliwa na wadau na TEF.
Makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk.Zainabu Chaula, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Jim Yonazi na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, leo Novemba 16, 2021 jijini Dodoma, Waziri Dk.Kijaji amesema Serikali inatekeleza kwa vitendo yale ambayo imeyaahidi kwa kuandaa mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa Waandishi wa Habari.
“Kwa uzalendo wetu kwa ushirikiano wetu tunatekeleza yale tuliyoaahidi kuyatekeleza kwa kuandaa mazingira rafiki, mimi kama Waziri wa Habari hii ni kazi yako Mwenyekiti (Deodarus Balile) na wadau na kila mmoja kujenga Taifa letu.
“Hakuna mtu anayetekeleza kwa ajili yake bali wote tufahamu tunatekeleza kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu,” amesema Dk. Kijaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa (TEF) Balile imeishukuru serikali kwa kuwa na sheria bora ambazo zitaondoa malalamiko ya muda mrefu.
Hata hivyo, amesema wanaomba kuwe na chombo kimoja ambacho kitaendesha tasnia ili kuepuka migongano, pamoja na kuangaliwa kwa muundo wa vyombo vya habari ambavyo vitaendesha tasnia hiyo.
“Tunaona ni vyema tuwe na chombo kimoja ambacho kitaendesha tasnia kuepuka mgongano mtarajiwa kwa sababu unaweza kukuta chombo hichi kimeamua hivi na majukumu mengi yalikuwa yanagongana.
“Kwenye sheria ilikuwa inaanzisha vyombo vinne ambapo tumekuja na mapendekezo ya kuomba kwamba kama zilivyotasnia zingine zinaendeshwa na chombo kimoja lakini tukabaini kwamba hatuwezi hata siku moja kugusa Mamlaka ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kwa sababu ukiangalia majukumu yake yapo kwa ajili ya ‘branding’ ya serikali.
“Kwa hiyo tumeyaleta mapendelezo haya tunaomba muyaangalie hatulazimishi kusema tulichokileta ndicho kiwe lakini kwa sasa tuna sheria bora,”amesema Balile.