23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru| Sekta ya Habari imechanua Tanzania

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema miaka 60 baada ya Uhuru Taifa limeshuhudia ukuaji wa sekta ya Habari ambapo kwa sasa kuna magazeti na machapisho yaliyosajiliwa 270, Radio zaidi ya 200, Vituo vya Televisheni  48, Blog 122, Radio mtandao zaidi ya 20.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 16,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Ashatu Kijaji wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ambayo Wizara hiyo imeyapata katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Dk. Ashatu Kijaji

Waziri Kijaji amesema  miaka 60 baada ya Uhuru Taifa limeshuhudia ukuaji wa sekta ya Habari ambapo kwa sasa kuna magazeti na machapisho yaliyosajiliwa 270, radio zaidi ya 200, Vituo vya televisheni  48, Blog 122, radio mtandao zaidi ya 20.

Amesema Taifa limeshuhudia  ukuaji na mabadiliko ya teknolojia nchini ambao umepelekea kuwa na Television Mtandao (online TV) zaidi ya 500 hadi sasa.

“Idadi hii ya vyombo vya habari inaonesha jinsi gani Taifa letu limepiga hatua kubwa katika kurahisisha na kuimarisha uhuru wa upatikanaji wa habari kwa wananchi wetu.

“Hivyo basi sote tutakubaliana kwamba kuna mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru yanayogusa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hapa nchini,  yanayohusisha utoaji wa taarifa mbalimbali za Serikali za kitaifa na kimataifa, taarifa za uchumi, siasa, michezo na burudani kwa wananchi kupitia redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii,”amesema Dk. Kijaji.

AVISHUKURU VYOMBO VYA HABARI

Waziri Kijaji amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kutoa habari, kuburudisha, na kuelimisha jamii juu ya matukio na masuala mbalimbali yanayojiri ndani na nje ya Nchi na kuchangia katika kukuza na kuimarisha demokrasia na utawala bora.

“Wizara ya Habari; Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatambua mchango wenu katika kuwaelimisha na kuwafikishia wananchi taarifa zinazohusu masuala mbalimbali ikiwemo Sera, Mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Hivyo basi napenda kuwapongeza kwa kazi hii ya kizalendo mnayofanya na ni imani yangu kuwa mtaendelea kufanya kazi zenu kwa moyo wa uzalendo na kuzingatia weledi katika kuiletea nchi yetu maendeleo hususani kupitia sekta hii adhimu ya Habari,”amesema Dk. Kijaji.

Amesema Mwaka 1993 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona umuhimu wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, iliamua kufungua milango na kuruhusu kuanzishwa kwa televisheni, redio na magazeti ya binafsi.

Amesema Kamisheni ya Utangazaji ilianzishwa Novemba 1993 chini ya Mwenyekiti wake  Mark Bomani na kuanza majukumu ya kupokea maombi na kutoa leseni za redio na televisheni, kufuatilia na kusimamia urushaji wa matangazo ya redio na televisheni pamoja na kufuatilia na kutoa masafa kwa vyombo vya utangazaji vya binafsi.

MKONGO WA TAIFA

Amesema kuwepo kwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye uwezo na ubora mkubwa unaoruhusu watoa huduma wote kuutumia bila upendeleo, kumeleta faida nyingi nchini.

Amezitaja faida hizo ni pamoja na kushuka kwa gharama za maunganisho ya jumla (interconnection fee) kwa simu za mkononi kutoka Sh 115 kwa dakika mwaka 2009 hadi Sh 10.4 mwaka 2020.

“Punguzo hili limewezesha kushuka kwa gharama za watumiaji wa mwisho na hivyo kufanya huduma za mawasiliano kutumiwa na wananchi wengi,” amesema.

Amesema ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano unaoonekana kwenye ongezeko la matumizi ya simu za mkononi, intaneti, miamala ya kifedha na ongezeko la mifumo mbali mbali ya kutolea huduma kwa njia ya mtandao.

“Mathalani mnamo tarehe 9 Disemba 1961 wakati wa Uhuru Tanganyika ilikuwa na simu za mezani 16,238 zilizokuwa kwenye matumizi Tanganyika nzima, nyingi zilikuwa za taasisi na idara za Serikali,”amesema.

Amesema hadi Juni 2021, kulikuwa na laini za simu za mkononi 53,111,246 na za mezani 71,405. Watumiaji wa intaneti wamefikia 29,152,713 ambao kabla ya uhuru hawakuwepo;

MINARA

Amesema hadi sasa Tanzania kuna jumla ya minara ya mawasiliano 12,902 ambapo minara 2,630 inatoa huduma ya 2G pekee na minara 9,579 inatoa huduma ya mawasiliano ya 2G, 3G au/na 4G.

Amesema UCSAF imejenga minara 1,068 kati ya minara tajwa hapo juu kwa kutumia ruzuku ya Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo hadi sasa takribani shilingi bilioni 161 zimetumika kujenga minara hiyo.

“Hivyo, ujenzi wa minara ya mawasiliano umefanyika kwenye kata 2,579 za Tanzania Bara kati ya kata 3,956 ambazo ni sawa na asilimia 65 na kwa upande wa Zanzibar, minara hiyo imejengwa kwenye kata 101 kati ya kata 110 ambazo ni sawa na asilimia 92.,”amesema.

Amesema Serikali katika azma yake ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ya uhakika na kwa gharama nafuu, Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, hivi karibuni imetangaza zabuni ya Sh bilioni 37.7 za ujenzi wa minara 224 ya mawasiliano katika maeneo ya kimkakati na mipakani.

 UKUAJI WA POSTA NA MZEE RAJABU YUSUFU

Aidha,Waziri Kijaji amesema   kabla ya Uhuru na mara baada ya Uhuru huduma za posta zilikuwa zinatolewa kwa kutumia watu waaminifu waliochaguliwa na jamii walioitwa mail runners.

Amemtolea mfano Mzee Rajab Yusufu aliyefanya kazi hiyo kwenye vituo viwili kati ya Nzega na Itobo halafu Itobo na Bukene vilivyopo mkoa wa Tabora.

“Mzee huyo alifanya mitihani wakati wa posta ya mkoloni, alifaulu na kuwa Afisa Msaidizi wa Posta, Tabora Mjini wakati wa mkoloni na baadae alijiendeleza na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Posta Tanzania baada ya nchi kupata Uhuru na baadae kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal unioni  PAPU),”amesema Dk. Kijaji.

Amesema ili kuhakikisha Wananchi wananufaika na uwekezaji mkubwa ulitokana na mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye eneo la Mawasiliano na Teknolojiaya Habari,  Mwaka 2010, Serikali ilianza kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.

“Mfumo huu unatambulisha mahali halisi ambapo mtu anaishi, mahali ilipo biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na Postikodi.

“Postikodi au simbo za posta kama inavyotambulika ni mfumo maalum wa tarakimu unaotambulisha eneo la kufikisha huduma za posta ambapo kwa nchi ya Tanzania inaanzia katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kanda,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles