NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WANAWAKE wameshauriwa kuondoa wasiwasi juu ya taulo za kike zinazotumika zaidi ya mara moja wakati wa kipindi cha hedhi.
Rai hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Malikia, Jenipher Shigoli ambaye ni mbunifu na mtenenezaji wa taulo hizo.
“Nilibuni taulo hizi baada ya kuona adha wanayokutana nayo wasichana waliopo shuleni, hasa katika maeneo ya vijijini. Niligundua kwamba wengi wanashindwa kununua taulo zile zinazouzwa huko madukani, hivyo wanapofika kipindi cha hedhi huona heri wasiende shuleni kwa hofu ya kuaibika.
“Nilifanya utafiti katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Iringa ambako nilihoji pia walimu, wakaniambia ni hali inayowakumba wasichana wengi, wapo ambao hulazimika kutumia magunzi, udongo, soksi, manyoya ya kuku kwa nia ya kujisitiri.
“Kwa hiyo nilikaa na wenzangu nikawaeleza kuwa tukitengeneza taulo hizi zitasaidia wazo ambalo limetimia miezi sita baadaye,” alisema.
Alisema taulo hizo zimetengenezwa kwa pamba pekee na kuwekwa nailoni maalumu kwa ustadi wa hali ya juu, ambayo huweza kupokea hadi kiwango cha milimita 30 hadi 40 za damu ya hedhi.
“Uwezo wake unalingana na zile taulo nyingine zinazouzwa huko madukani na huweza kuvaliwa kati ya saa sita hadi saba. Baada ya saa hizo unalazimika kuifua na kuianika ikauke vizuri kwa kuitumia tena na hudumu hadi mwaka mmoja,” alisema.
Shigoli ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu kwa kumwezesha mtaji wa Sh milioni 30 kukuza biashara yake hiyo.
“Walinisaidia pia kupata eneo ambalo natarajia kujenga kiwanda kikubwa ambacho kitazinduliwa Machi mwaka huu huko Kibaha mkoani Pwani,” alisema.
Alisema kupitia bidhaa yake hiyo aliweza kuibuka mshindi katika shindano la kusaka wabunifu barani Afrika mwaka jana linalosimamiwa na Taasisi ya African Entrepreneur Award.
“Niliibuka mshindi wa kwanza na nilizawadiwa Dola 150,000 (sawa na Sh milioni 300) za Tanzania, nimeshapeleka barua Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambako natarajia kupata ushirikiano ili nisaidie jamii yangu,” alisema.