23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tatizo si Malinzi wala TFF, kikwazo ni mfumo

rais-wa-shirikisho-la-mpira-wa-miguu-jamal-malinziNa HAMIS MWINYI

WADAU wanasema soka la Tanzania limeanguka! Wanasema soka halina mwelekeo! Ni hakika yenye walakini ambayo haipambanuliwi wazi juu ya wahusika halisi wa matatizo au kudumaa kwa soka nchini.

Ni vigumu kulituhumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusika moja kwa moja, tusijaribu kuuficha ukweli.

Tafsiri ya maelezo hayo inazingatia vigezo vya kufuta au kuvunja taasisi za michezo kwenye mashirika, makampuni, viwanda na idara za Serikali ambavyo kwa hakika ndio chanzo kikuu cha anguko la ustawi na maendeleo ya soka la Tanzania, hasa linapofikia ngazi ya kimataifa. Yupo anayebisha juu ya hili?

Bila shaka hakuna. Maana yake hata kwenye sekta ya elimu pia kumepoteza kabisa sifa ya kuwa chachu muhimu ya kuibua vipaji tangu ngazi za mashuleni.

Ndiyo! Huko mashuleni ndiko vilikoonekana vipaji na watoto walipofikia umri wa kuajiriwa walitumika katika timu za mashirika, makampuni, viwanda na idara mbalimbali za serikali.

Tukirudisha kumbukumbu zetu nyuma takriban miaka ishirini iliyopita, tutaafikiana na makala haya kuwa wachezaji wa michezo wazuri na hata wasanii wengi waliowika enzi hizo walitokana na timu au vikundi vilivyokuwa vikimilikiwa na mashirika, viwanda, makampuni, idara na taasisi za Serikali ambazo kwa sasa hazina kabisa timu au vikundi na kama zipo zinahesabika.

Bila kupepesa macho wala ujanja ujanja, lazima tukubaliane kuwa, kufa kwa mashirika, makampuni na viwanda vingi nchini ndio chimbuko la kweli la anguko hilo ambalo haliishii kwenye soka tu, bali hata vikundi vya sanaa kama ngoma, maigizo, ngonjera nk. Unawezaje kuwasahau Mzee Jongo, Pwagu na Tambalizeni?

Ni nani aliyekuwepo enzi hizo asiwe na kumbukumbu ya timu za Sigara, Pilsner, Kurugenzi ya Dodoma, Pamba ya Mwanza, Ushirika ya Moshi, Reli ya Morogoro, Biashara ya Shinyanga, RTC Kagera na Kigoma? Zote hizo zilishiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na nyingine kibao kutaja chache. Zilikuwepo mpaka timu za michezo mingine kama ngumi na netiboli. Tumezisahau timu za Bandari, Bima, Tanesco nk?

Hata tukienda upande wa pili wa sanaa, bila shaka tutakumbuka vikundi kama DDC Kibisa, Bima Taarab na vingine mpaka baadaye ikazaliwa TOT. Miaka hiyo palikuwa na kila kitu kuibua, kukuza na kusimamia vipaji vya michezo na sanaa takribani aina zote. Wasimamizi na walezi walikuwepo na ndiyo maana kukawa na hamasa na mshawasha mkubwa kwa Watanzania.

Kinachoiponza nchi hii ni mabadiliko au kufa kwa mfumo wa kuwa na timu au vikundi katika taasisi tajwa hapo juu. Bahati mbaya zaidi serikali haijaonesha nia ya dhati ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili zaidi ya kubaki nyuma na kusikiliza vilio na manung’uniko ya wadau kwa masikio yaliyozibwa pamba.

Kama hufikirii kwa makini, lazima umuangushie lawama Jamal Malinzi, ambaye ndiye Rais wa TFF, lakini, kama utatafakari kwa kina, hapana shaka utabaini na kusadiki maelezo ya makala haya kwamba mfumo uliopo ndio tatizo kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles