Samwel Mwanga-Maswa
Ukosefu wa taulo za kike katika shule za msingi wilaya ya Maswa mkoani
Simiyu limeendelea kuwa tatizo kwa wanafunzi wa kike hali inayopelekea kushindwa kuhudhuria masomo wakati wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wanafunzi wa kike walioko katika kambi ya
kitaaluma katika shule ya msingi Binza iliyopo wilayani hapa kwa wanafunzi wa darasa la saba walipokuwa wakizungumza na MTANZANIA
ilipowatembelea katika kambi hiyo kuona changamoto zinazowakabili.
Walisema kuwa sasa umefika wakati kwa serikali kuweka utaratibu
madhubuti utakaowawezesha kupata hitaji hilo maalum lenye msingi wa
kulinda afya zao.
“Ni lazima sasa tufunguke juu ya suala hili la taulo za kike
kuwepo
katika shule zetu za msingi wanafunzi wa kike hatuna haja ya
kuficha
ni lazima tuwe wazi kwani tunaathirika sana kwa kukosa
vipindi tunapokuwa katika kipindi cha hedhi hivyo ni vizuri
serikali
ikaona umuhimu wa kuweka bajeti ya kununua taulo hizo katika
shule
zetu iwe ni sehemu ya sisi kupata elimu bila malipo,” amesema
mmoja wa wanafunzi Fatuma Ally.
Aidha wanafunzi hao wamesema kuwa licha ya
utaratibu mzuri uliowekwa na serikali ya mkoa wa Simiyu ya kuwaweka katika makambi hayo lakini zipo
sababu nyingi zinazochangia
kudumaa kwa ustawi wa elimu ya mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na uhaba wa taulo za usafi wakati wa hedhi
kwani wanakuwa na hofu ya kupoteza
thamani ya utu wao hasa shuleni.
“Hali hii hutufanya baadhi yetu kutohudhuria darasani na
matokeo yake wengine wasio wavumilivu hufikia
uamuzi wa kuacha shule
na taifa litakosa wasomi mahiri kwa siku zijazo,” amesema
Magreth
Joseph.