27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TASAC yaeleza inavyodhibiti ukwepaji kodi sekta ya meli

Na Clara Matimo, Mwanza

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), limesema udhibiti makini wa sekta ya usafirishaji majini, mazingira  baharini na nyaraka zinazoleta mizigo na kupeleka mizigo nje ya nchi,  unasaidia kuondoa ukwepaji kodi hivyo  mapato yatokanayo na shughuli za meli kuongezeka.

Hayo yameelezwa na TASAC, Nelson Mlali wakati akizungumza na MTANZANIA Digital kwenye maonesho ya 16 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea kwenye viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza.

Mlali amebainisha kuwa ni kazi muhimu kwani inadhibiti kiwango cha mizigo tangu kinavyotoka huko hadi kinapoingia nchini pasipo kufanyiwa ujanja wowote wa kupunguza hali inayowezesha  serikali  kukusanya kodi kutokana na kiwango halisi na kuepusha mianya ya uhujumu mapato.

Amesema baadhi ya wasafirishaji wamekuwa na tabia ya kupunguza nyaraka na kudanganya kiasi cha mizigo iliyobebwa na kuikosesha mapato serikali, lakini kwa sasa wamedhibiti ambapo nyaraka zinapitia kwao kisha huwapa mawakala wa meli waliopo nchini ambao huzipeleka kwenye mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

“Baadaye tunazunguka tunaenda TRA kuangalia kama tulichowapa wakipeleke kule ndicho walichopeleka au walifanya ujanja wowote,  lengo ni kudhibiti mapato ya Serikali, hii kazi ni muhimu kwa sababu tunapunguza ujanja unaoweza kuikosesha serikali mapato.

“Suala la udhibiti wa nyaraka ni kwamba mizigo inapotumwa kuja nchini nyaraka zote zinatumwa kwetu kwanza halafu sisi tunazipa control ndipo tunazipeleka kwa mawakala waliopo nchini ili waweze kuendelea na taratibu zingine za kiforodha ,” amesema Mlali.

Ameongeza kwa kueleza kuwa mfanyabiashara atakayeenda kinyume na hiyo atatozwa faini ya Dola za Kimarekano 20,000 hadi 40,000 ili iwe funzo kwa wengine kwani tozo hiyo ni kubwa na inawezesha kusababisha uzembe wa mtu mmoja ukaigharimu kampuni na ikafungwa.

Akieleza majukumu mengine ya taasisi hiyo, Mlali amesema kuwa  ni kazi za uwakala wa forodha kwenye maeneo mahususi ambayo ni nyeti katika uchumi wa nchi, uhakiki wa shehena zinazopanda na kushuka melini ili serikali itambue ni nini kimeingia nchini na kipi kimetoka kwenda nje ya nchi, kufanya kazi ya uwakala wa meli kwa baadhi ya meli zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria ambazo ni meli za mafuta, kijeshi za kokodiwa na zinazofanya utafiti katika bahari labda  wa mafuta na meli zinazoleta magari.

“Serikali imetoa majukumu hayo kwa TASAC ili tusimamie vizuri maeneo hayo kuhakikisha usalama wa nchi na kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa usahihi,”amesema Mlali na kuongeza

“Kwa upande wa udhibiti tunaudhibiti wa aina mbili, udhibiti wa sekta nzima ya usafiri wa majini kwa kuangalia tozo zinazotozwa na kama watoa huduma katika bandari wanatoa huduma bora.

“Udhibiti  kwenye sekta ya usafiri majini  tunaangalia usalama wa vyombo, uwezo wa manahodha wanaoviendesha vyombo hivyo na ndiyo maana wanapotoka chuoni na sisi tunawapa mitihani halafu tunawapa vyeti vyetu ambavyo vinatambulika kimataifa, pia tunaangalia usafi katika maeneo ya majini ili usafiri wa majini ikiwemo meli visisababishe uchafuzi wa mazingira katika nchi,” amesema

Kaimu Meneja  Masoko na Uhusiano wa umma TASAC, Josephine Bujiku, amesema maonesho hayo ni muhimu kwao maana yanawasaidia kutoa elimu kwa wananchi na wadau wao  kuhusu huduma mbalimbali wanazozitoa vilevile wanapata fursa ya kupokea  maoni pamoja na  mapendekezo.

 “Tunafurahi pia wanapotuuliza maswali mbalimbali ambayo tunayajibu kwa kweli manonesho haya  ni sehemu muhimu kwetu maana tunakutana  ana kwa ana na wadau wetu pamoja na wananchi ambao walipenda kukutana na sisi lakini kutokana na umbali labda walishindwa kutufikia ingawa tunaofisi katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini.

“Ila kwa kutambua umuhimu wa wadau wetu tunatumia njia mbalimbali ambazo zinatusaidia kutoa elimu  na taarifa mbalimbali  zinazojitokeza mara kwa mara kwao ikiwemo machapisho, mabango, mitandao ya kijamii na  vyomba vya habari,” amesema Bujiku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles