28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa bilioni 15 kununua mahindi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeshatoa bilioni 15 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Septemba 2, 2021, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwela, Deus Clement Sangu katika  kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Uzalishaji wa mahindi ni mkubwa lakini na sisi pia tumeimarisha hifadhi yetu ya Taifa ya chakula. NFRA tumeipa fedha za kwenda kununua mahindi kwa bei ya kumwezesha mkulima ili ajikimu hadi msimu ujao. Uwezo si mkubwa sana, lakini tumetoa shilingi bilioni 15,” amesema.

Majaliwa amesema siku nne zilizopita alikuwa ziarani mkoani Katavi na aliona hali halisi ya mlundikano wa mahindi na akakutana na watu wa NFRA ili aone kasi yao ya ununuzi ikoje.

“Nilibaini kuwa uwezo wao ni mdogo na nikapokea malalamiko ya wananchi kwamba kituo cha kupokelea mahindi kiko mbali, kwa hiyo tumeamua kuanzia sasa kila Halmashauri itapaswa iwe na kituo japo kimoja cha kupokelea mahindi ili kuharakisha ununuzi wa zao hilo.

“Tunawahakikishia wakulima wetu kwamba tunanunua mahindi kupitia NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko na pia tumefungua milango kwa yeyote anayetaka kuuza mahindi nje. Mtu akitaka kuuza mahindi Zambia, Congo, Msumbiji au Malawi yuko huru kufanya hivyo ili mradi atoe taarifa ili nasi tujue tumeuza kiasi gani,” amesema wakati akimjibu Sangu ambaye alitaka kujua Serikali imejipanga vipi kuziwezesha taasisi za Serikali kama NFRA ili ziweze kununua mahindi ya wakulima?

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuunganisha taasisi za NIDA na RITA kutokana na tofautiana majukumu yake.

Alikuwa akijibu swali la Abubakari Damian Asenga, mbunge wa Kilombero ambaye alishauri taasisi hizo ziunganishwe ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ambavyo alisema kwa sasa vinacheleweshwa.

“NIDA inatoa kitambulisho cha Taifa ambacho kinamtambulisha Mtanzania na hakitolewi kwa mtu ambaye si raia wakati RITA inatoa cheti cha kuzaliwa kikionesha kuwa umezaliwa wapi, tarehe yako ya kuzaliwa na pia wanatoa cheti cha kifo.”

Majaliwa amesema RITA inaweza kutoa cheti cha kuzaliwa kwa mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania kwa sababu pale hospitalini akishazaliwa mtoto, taarifa zitaonesha hivyo na inaweza kutoa cheti kwa huyo mtoto  hata kama siyo Mtanzania.

“Mtu anaweza kuzaliwa Tanzania na kupewa cheti cha kuzaliwa kwa kuwa amezaliwa ndani ya nchi yetu, lakini mtu huyo anaweza asiwe Mtanzania kwa mujibu wa sheria zetu,” amesema.

Amesema taasisi hizo zinaweza kupeana taarifa pale inapobidi lakini vyote vina majukumu tofauti. “Urasimu unaosemwa hapa nimeusikia wakati nilipofanya ziara kwenye mikoa ya pembezoni na huko nimekuwa nikisisitiza umakini katika kuchunguza taarifa za waombaji.

“Kuchelewa kwetu kwenye mikoa ya pembezoni ambako pia kunaitwa urasimu, kunafanywa kwa nia nzuri ili kujiridhisha kama kweli anayeomba kitambulisho ni raia wa Tanzania.

“Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba mtu yeyote Mtanzania ambaye baba na mama ni Watanzania, ni lazima atapata kitambulisho cha Taifa, kikubwa wawe na subira. Nasi kwa upande wetu tumejitahidi kuongeza vifaa na watumishi ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo hasa kwa wale ambao wamehakikiwa na wanastahili,” amesisitiza Waziri Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles