Na Yohana Paul, Mwanza
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Uvuvi na Mifugo wameanza utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Vyombo Vidogo vya Usafiri Majini katika mialo mbalimbali jijini Mwanza.
Akitoa taarifa ya sensa hiyo, Afisa Uhusiano Mwandamizi TASAC , Amina Miruko amesema zoezi hilo litafanyika kwenye maeneo yote mkoani Mwanza na Tanzania Bara ili kupata takwimu za jumla kitaifa.
Amesema kabla ya kuendesha zoezi hilo yametolewa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Uvuvi Tanzania Bara yaliyohusisha watendaji wa TASAC, NBS na Maafisa Uvuvi kutoka mikoa mbalimbali.
Amesema lengo kuu la sensa hiyo ni kutaka kujua idadi ya vyombo vidogo vya Usafiri Majini ili kutengeneza kanzidata itakayosaidia katika kupanga maendeleo ya kiusalama na kiuchumi katika Taifa.
Aidha wamiliki wanaombwa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TASAC, NBS na Wizara ya Uvuvi kwani adhima ya serikali ni kuweka serikali ina dhamira njema.