Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
TIMU ya soka ya Tanzania kwa watu wenye ulemavu, Tembo Warriors, imefanikiwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 zitazofanyika Uturuki baada ya leo Desemba Mosi, kuichapa Cameroon mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao hayo yamefungwa na Alfan Kyanga aliyefunga mawili dakika 2,15, Ramadhan Chomole dakika ya 18 na Frank Ngailo dakika ya 36, 44.
Tembo Warriors imefuzu Kombe la Dunia baada ya kutinga nusu fainali ya michuano ya Afrika wa wenye ulemavu (CANAF 2021) inayoendelea jijini ambapo imekuwa timu ya kwanza kufuzu kati ya nne zinazotakiwa kwa Afrika.
Mchezo huo umeshuhudiwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Innocent Bashungwa na Rais wa Mashindano hayo duniani Mateus Wildack na viongozi wengine wa wizara hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo, Bashungwa amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuisaidia timu hiyo katika maandalizi ya Kombe la Dunia ili iendelee kufanya vizuri.