25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah amshukuru Rais Samia ujenzi wa madarasa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha jimbo hilo kupata sh bilioni 1.7 za ujenzi wa vyumba vya madarasa 86 katika kata nane.

Jimbo hilo lenye kata 13 lina shule za sekondari 17 na awali lilikuwa na upungufu wa vyumba 125 hali iliyosababisha wanafunzi kusoma kwa awamu katika baadhi ya shule.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba hivyo amesema hivi sasa watakuwa na vyumba 506 kutoka 420 na kwamba watabaki na upungufu wa vyumba 39.

“Mheshimiwa Rais amefanya jambo kubwa sana na hili ndilo limetufanya tusikae kimya, tunamshukuru sana na tunawaomba Watanzania tuungane ili tumuombee rais wetu kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwa na afya njema aendelee kutuletea maendeleo zaidi,” amesema Bonnah.

Mafundi wakiendelea na ujenzi katika Shule ya Sekondari Kiwalani ambako kunajengwa vyumba 12 vya madarasa.

Amesema watahakikisha wanashirikiana na viongozi wote kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi mkoa pamoja na wadau wa maendeleo ili kujenga vyumba vilivyobaki na kuondokana kabisa na upungufu jimboni humo.

Aidha amesema tayari watoto 6,893 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kufanya idadi ya wanafunzi wote kufikia 26,860 kwa ikama ya kukaa 45 hadi 50 kwa kila darasa.

Mbunge huyo amekagua ujenzi wa madarasa hayo katika Shule ya Sekondari Magoza iliyopo Kata ya Kisukuru, Zawadi (Tabata), Binti Musa (Minazi Mirefu), Kiwalani (Kiwalani), Buguruni Moto (Buguruni), Majani ya Chai na Minazi Mirefu (Kipawa).

“Tumefanya ziara katika shule zote ambako kunajengwa vyumna vya madarasa na tumejionea hali halisi maendeleo ni mazuri maeneo mengi wanapaua,” amesema.

Naye Diwani wa Kata ya Kisukuru Lucy Lugome, amesema ujenzi wa vyumba vitano katika Shule ya Sekondari Magoza vinavyogharimu Sh milioni 100 umefikia katika hatua ya kupaua na kuahidi kuwa yatamalizika katika muda uliopangwa.

Mwalimu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari Kiwalani, Juma Mohamed, amesema wamepokea Sh milioni 300 na kwamba wanajenga madarasa 12 na fedha nyingine zitatumika kujaza kifusi katika eneo korofi shuleni hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amewataka mafundi kuongeza kasi ya ujenzi na kuwaagiza wakuu wa shule kuanza kujipanga kwa ajili ya madawati.

“Wilaya yetu imefanya vizuri mwaka huu watoto 26,000 wamefaulu, miaka ya nyuma ilikuwa watoto wanachaguliwa kuanza kidato cha kwanza kwa awamu lakini safari hii wote wataanza pamoja,” amesema Ludigija.

Kuhusu ombi la kuwa na shule ya kidato cha tano na sita amesema watajitahidi ipatikane kupitia mapato ya ndani au kufanya marekebisho katika bajeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles