Na Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Nchini (TCT), Abdulikadir Mohamed, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha wazo la kuwa na tamasha la urithi wa Mtanzania maarufu Urithi Festival litakalokuwa linafanyika kila mwaka.
Mohamed ameyasema leo Jumatatu Oktoba Mosi, wakati akizindua tamasha hilo kwa mwaka huu kwa jiji la Dar es Salaam.
Amesema lengo la tamasha hilo ni kuendeleza na kutangaza alama na tunu za taifa ili kudumisha umoja na uzalendo wa taifa, kuenzi na kunadi utalii kama hazina kuu ya utamaduni wa malikale.
“Katika kipindi cha miaka 57 ya uwepo wa Taifa letu, tumepata mafanikio mengi makubwa katika kulinda na kuendeleza maliasili na malikale zetu ikiwamo kulinda na kuthamini muungano wetu na lugha yetu ya Kiswahili,” ameseama Mohamed.
Tamasha hilo lililoanza rasmi leo katika Mkoa wa Dar es salaam litafanyika kwa siku sita ambapo litahitimishwa Jumamosi Oktoba 6, mwaka huu.