NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imefanikiwa kurejesha serikalini zaidi ya Sh bilioni 14.69 kutoka kwa watu iliyosema ni mafisadi.
Fedha hizo zimerejeshwa kuanzia mwaka 2016 hadi sasa sambamba na nyumba saba na magari manne yaliyotaifishwa.
Akizungumza jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman, alisema pia wameweka zuio la mali zikiwamo akaunti zenye zaidi ya Sh bilioni 20, nyumba 26, viwanja 47, magari 61 na mashamba 13.
“Tunayo mamlaka kwa kufuata sheria ya kutafuta, kushikilia na kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa au zilizotokana na mazalia ya rushwa, hata kama mhusika atakuwa amefariki,” alisema Kamishna Diwani.
Alifafanua kuwa baada ya hatua za ufuatiliaji na ushikiliaji, huwasilisha mahakamani maombi ya kutaifisha mali husika kwa kufuata taratibu za sheria.
Alisema kulingana na marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya 2016, makosa yote ya rushwa sasa yamekuwa ya uhujumu uchumi na sheria imeipa mamlaka mahakama kutoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 20.
“Suala la urejeshaji wa mali ni takwa la kisheria kulingana na mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mapambano dhidi ya rushwa wa mwaka 2003. Tunataka kuhakikisha mali husika zinapatikana pale ambapo mahakama itakapotoa amri ya kuzitaifisha,” alisema.
UTAKATISHAJI FEDHA
Katika hatua nyingine, Takukuru ilitangaza kumtafuta mkazi wa Kinondoni, Magreth Kobelo Bonzaga, anayetuhumiwa kutakatisha fedha haramu na kujipatia mali.
Tangazo hili limetolewa kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupitia shauri la jinai namba 28 la mwaka 2019.
Kamishna Diwani alisema kuanzia juzi walianza kutoa matangazo ya kumtafuta mtuhumiwa huyo kupitia vyombo na majukwaa mbalimbali ya habari.
Alisema mtuhumiwa huyo alijipatia mali hizo kupitia Kampuni ya Suprio Financing Solution Ltd (SFS) iliyokuwa inafanya biashara pasipo kulipa kodi ya Serikali.
“Tunategemea kuiomba mahakama ziwe mali za Serikali iwapo hatarudi nchini kujibu tuhuma zinazomkabili. Tunamtafuta kokote duniani, lengo ni kutaka haki itendeke kwa sababu hatutaki kumwonea mtu,” alisema Kamishna Diwani.
Alisema katika nyakati tofauti mtuhumiwa huyo alinunua viwanja vitatu vilivyoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi na nyumba tatu zilizoko Tegeta, Manispaa ya Kinondoni.
Alivitaja viwanja hivyo vilivyoko Amani Govu, Manispaa ya Temeke kuwa ni kiwanja namba 191 block B, kiwanja namba 176 block B na kiwanja namba 174 block B.
Kwa upande wa nyumba ambazo zote ziko Tegeta, Manispaa ya Kinondoni, alisema ni zenye namba 200 block D, 1378 block E na 196 block D.
Alisema wakati uchunguzi ukiendelea, mtuhumiwa huyo alitoroka nchini ndiyo maana wameamua kutangaza kutafutwa kabla ya kutaifisha mali alizojipatia kwa rushwa.
“Asiporudi nchini kwenye kesi inayomkabili madhara yake ni makubwa sana kwake binafsi na familia yake, kwa kuwa mali zitataifishwa na kurudishwa serikalini kwa mujibu wa sheria.
“Ukijihusisha na vitendo vya rushwa hutakuwa umepata bali utakuwa umepatikana, utakumbana na mkono wa Takukuru ikiwemo kufungwa jela na kutaifishiwa mali zote ulizozipata kwa rushwa,” alisema Kamishna Diwani.
Taasisi hiyo pia iliwaonesha waandishi wa habari mojawapo ya nyumba inayodaiwa kuwa ni ya mtuhumiwa huyo iliyopo Tegeta, Manispaa ya Kinondoni.
Nyumba hiyo ya kifahari ina bwawa la kuogelea, viwanja vya michezo na kwa ndani ina sehemu ya kuoneshea sinema.