27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yatangaza kuanza majaribio usajili wapigaKura

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kuanza kuandikisha  wapiga kura kwa majaribio katika kata mbili za Kibuta wilayani Kisarawe na Kihonda katika Manispaa ya Morogoro.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Semistocles Kaijage,  Dar es Salaam jana imeeleza kuwa uandikishaji huo wa majaribio utaanza Machi 29, hadi Aprili 4, mwaka huu utafanyika katika vituo 20 vya kuandikisha wapiga kura ikiwa ni vituo 10 katika kila kata. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uandikishaji huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa uandikishaji wapiga kura   kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi kwa hatua hiyo.

NEC imetaja sifa za watu watakaoandikishwa katika uandikishaji huo kuwa ni raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 au atakayetimiza umri wa miaka 18 siku ya Uchaguzi  Mkuu ujao.

Uandikishaji huo hautawahusu raia walio chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine, aliyebainika kuwa hana akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa akili au yuko kizuizini kwa ridhaa ya rais.

“Watu ambao hawatahusika katika majaribio hayo ya kuboresha kuwa ni mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo kinachozidi miezi sita  na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote inayohusu makosa ya uchaguzi.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia inawajulisha wakazi wa kata hizo zinazofanya uandikishaji wa majaribio na ambao walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015 kuwa wanaweza kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao katika vituo walivyojiandikishia,” alisema Jaji Kaijage.

Wakati huo huo, NEC imetoa fursa kwa vyama vya siasa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikishia wapiga kura kwa lengo la kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika pamoja na changamoto zitakazojitokeza  ziweze kupatiwa ufumbuzi kabla ya hatua rasmi ya uandikishaji.

Kutokana na hali hiyo vyama vimetakiwa kuwasilisha nakala mbili za barua za utambulisho zikiwa na picha mbili na nakala mojawapo kati ya Kitambulisho cha Taifa au Kadi ya Mpiga Kura, Hati ya Kusafiria au Leseni ya Udereva na kwamba kila chama kitagharamia wakala wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wakati wa uandikishaji huo wa majaribio Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatumia runinga, redio, mitandao ya  jamii na magari ya matangazo kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura   kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika hatua hiyo.

Mwenyekiti huyo wa NEC amewaomba wakazi wa kata za Kibuta na Kihonda kujitokeza kwa wingi katika uandikishaji huo wa majaribio na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hilo muhimu kwa mustakabali wa demokrasia ya taifa.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi hufanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba inayoipa Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na wabunge   na madiwani kwa Tanzania Bara.

Tume, kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles