ACT, msajili jino kwa jino

0
2367
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kujibu hoja zilizotolewa kwenye barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka kukifuta cha hicho.Kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremiah Maganja.
  • Zitto atoa hoja tano kujibu masuala ya hesabu za   chama, udini, bendera za CUF kuchomwa
  • Jaji Mutungi atoa neno kukazia barua yake

ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuacha kukitisha chama hicho kwa kuwa ndiyo kwanza kinaanza upya, huku msajili kwa upande wake akisema anasubiri majibu yao ndipo azungumze.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zitto alisema barua ya msajili wa vyama vya siasa iliyotumwa kwa uongozi wa chama hicho juzi ni ishara ya dola kutikisika baada ya kumpokea aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mseto ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Kwa sababu ambazo msajili amezitoa, hakuwa na nia njema. Kule kwetu Kigoma huwa kuna msemo unaosema ukiona kifaranga kiko juu ya chungu, ujue mama yake yuko chini yake. Kwa hiyo Serikali isitujaribu, sisi wote ni Watanzania na watambue kuwa hakuna wa daraja A au B.

 “Tunajua hii inatokana na dola kuona kuwa haitaweza kushika uchaguzi wa 2020 kule Zanzibar kama walivyotarajia. Yule wanayemwogopa, Maalim Seif Shariff Hamad ni Mtanzania.

“Wamemfunga, wamemnyang’anya ushindi wake mara tano, wamemnyang’anya chama amewaachia, wajue sasa tuko imara baada ya kumpokea,” alisema.

Zitto alisema Serikali ilizoea kuwa vyama vikubwa Zanzibar ilikuwa CCM na CUF, lakini baada ya CUF kuvurugwa wananchi wameamua kuwaachia na kuifanya ACT-Wazalendo kuwa chama kikubwa upande wa Visiwani.

Alisema hatua za kujaribu kuifuta ACT-Wazalendo ni tishio kwa usalama wa nchi, hivyo ni vyema msajili afute barua hiyo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo, Zitto alisema hakuna ukweli katika suala la kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu za mwaka 2013/14 kwa kuwa chama hicho kilipata usajili wa kudumu Mei, 2015 ikiwa ni miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha wa Serikali.

Alisema kutokana na hatua hiyo, walishauriwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mujibu wa kanuni za uunganishaji wa hesabu, hivyo kuunganisha hesabu za miezi miwili kwenye hesabu za miezi 12 ya mwaka wa fedha wa Serikali uliofuata.

“Kabla ya kutekeleza uamuzi huo tuliomba idhini ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia barua zetu mbili, moja ya Januari 22 na nyingine ya Januari 29, 2015 na barua hizi zote zilijibiwa na huyu huyu Sisty Nyahoza, zikituruhusu kufanya hivyo. Huyu ndiye aliyetia saini barua tuliyoipata jana (juzi),” alisema.

Alisema baada ya hatua hiyo walitimiza wajibu wao wa kupeleka hesabu zao kwa CAG kwa ukaguzi, ambaye alizipitisha na kuzipiga muhuri wa moto kwenye nakala walizonazo na uongozi wa chama pia uliziwasilisha kwa msajili.

“Kama msajili angekuwa na nia njema, kama amepoteza hizi taarifa huko ofisini kwake angeweza tu kuuliza na tungempa taarifa zote kwa usahihi. Ieleweke kwamba wajibu wetu kwa mujibu wa sheria, kama chama cha siasa ni kuwasilisha taarifa kwa CAG kisha anakuja kukagua,” alisema.

Zitto alisema hawajawahi kuacha kuwasilisha taarifa zao kwa CAG tangu walipopata usajili wa kudumu na kwamba tangu kuanza kwa ukaguzi, chama chao pekee ndicho kilichopata hati safi katika hesabu zake.

Alisema kwa kuwa msajili si mhasibu wala si mkaguzi, alipaswa kuuliza au kushauriana na wahasibu katika ofisi yake na pia kuwasiliana na ofisi ya CAG kabla ya kuchukua hatua ya kuandika barua hiyo.

“Ninamshauri msajili afanye mambo anayoyajua, yale asiyoyajua awaachie wanaoyajua, aachane nayo,” alisema.

KUCHOMWA BENDERA ZA CUF

Kuhusu tuhuma za watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa ACT-Wazalendo walioonekana wakichoma bendera za CUF kupitia mitandao ya kijamii, Zitto alisema msajili anatakiwa kuwa na uhakika kuhusu wanachama anaowazungumzia, kwa kuwa chama chake kina utaratibu ulio wazi wa kuwatambua na kuwashughulikia wanachama wake.

Alisema ACT-Wazalendo ni chama rasmi kilichosajiliwa kisheria, kikiwa na utaratibu wake wa kusajili wanachama na kuwapa kadi, hivyo ni vyema msajili akawahakikishia kuhusu wanachama hao ili wawachukulie hatua za kinidhamu kama chama.

Kuhusu matumizi ya neno Takbir, ambalo msajili alidai linaonesha udini, Zitto alisema wanatoa nafasi kwa wanazuoni wamweleze msajili kuhusu matumizi ya neno hilo.

“Pamoja na kuwa Serikali haina dini, tumeona katika hafla mbalimbali viongozi wakianza kusalimia kwa kutumia maneno kama ‘Bwana Asifiwe’, ‘Tumsifu Yesu Kristo’, ‘Salaam Aleikum’. Ina maana hiyo nayo si sahihi?” alihoji.

Alisema ni vyema viongozi wa kidini wajitokeze waeleze maana ya matumizi ya maneno hayo, na kwa kuwa ofisi ya msajili haina sheikh, imamu wala mchungaji, Sheikh Mkuu ikiwezekana atangaze ‘Fatwa’ (mwongozo/uamuzi) kuhusu matumizi ya neno ‘Takbir’.

Zitto alisema chama chake kinafuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria na Katiba, watafuata utaratibu kwa kumwandikia msajili wa vyama kumjibu barua hiyo na kumpa vielelezo vyote, lakini ni vyema afikirie kuifuta barua yake kwa kuwa inamtia aibu.

Alisema kwa kuwa barua hiyo inaonekana wazi kuwa ina nia ovu, wanaitangaa kuwa tishio kwa usalama wa taifa na wataandika barua kwa jumuiya ya kimataifa, kuanzia kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kueleza malalamiko yao.

Zitto alisema pamoja na EAC, watauandikia uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya zote za kimataifa kuhusu tishio la kukifuta chama chao na tishio la usalama wa taifa kutokana na hatua hiyo ya msajili.

KAULI YA MSAJILI

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi alieleza kwa ufupi kuwa wanasubiri majibu ya barua hiyo kutoka kwa ACT-Wazalendo kwa ajili ya hatua zaidi.

“Tunasubiri majibu ya barua tuliyowaandikia, tutatoa taarifa kuhusu kinachoendelea,” alisema.

BARUA YA MSAJILI

Barua kwa ACT-Wazalendo iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ilitoa siku 14 kwa chama hicho kilieleze kwanini kisifutwe kwa mujibu wa sheria kutokana na kukiuka taratibu za usajili wake.

Kwa mujibu wa barua hiyo, tuhuma kwa chama hicho ni kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/14, hatua inayokiuka Sheria ya Vyama vya Siasa sura ya 258.

Tuhuma nyingine ni vitendo vya uvunjifu wa sheria, ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016 ambayo Profesa Ibrahim Lipumba alithibitishwa kuwa mwenyekiti wa CUF.

Barua hiyo ilieleza kuwa vitendo hivyo vilifanywa na mashabiki wa Maalim Seif, jambo ambalo ni kukiuka kifungu cha 11C cha sheria ya vyama vya siasa.

Ilisema tuhuma nyingine za chama hicho ni kutumia dini katika siasa baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo huku wakisema ‘Takbir’ kitendo walichosema kinakiuka kifungu cha 9 (1) (C) cha sheria hiyo.

Barua hiyo ilisema viongozi wa ACT-Wazalendo hawajaonekana wakikemea vitendo hivyo jambo linaloonesha chama hicho kinakubaliana navyo.

DUNI APEWA WADHIFA WA JUU

Katika hatua nyingine, Zitto amemtangaza rasmi mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji kuwa naibu kiongozi wa chama hicho, nafasi inayofuatia baada ya kiongozi wa chama.

Duni ambaye alihamia chama hicho wiki iliyopita, aliwahi kuwa mgombea mwenza wa aliyekuwa mgombea wa Chadema kupitia Ukawa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, Edward Lowassa.

Alilazimika kuhamia Chadema na kupitishwa kuwa mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho na baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, alirejea katika chama chake za zamani cha CUF.

Zitto alisema jana kuwa uamuzi wa uteuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha uongozi wa chama kilichofanyika juzi.

“Nimepewa mamlaka na katiba ya chama kumteua, nikawasilisha kwa uongozi na wameridhia na uteuzi wake utaanza rasmi kesho,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here