Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Wafanyabiashara wa zao la kahawa mkoani Kilimanjaro, wamefadika na elimu ya umuhimu wa upimaji wa mionzi katika zao hilo iliyotolewa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwenye soko la mnada uliofanyika wilayani Moshi mkoani humo.
Mnada huo uliofanyika leo Alhamisi Novemba 21, umewashirikisha wafanyabiashara mbalimbali wanaosafirisha kahawa ndani na nje ya nchi ambapo wamepata uelewa wa sababu za upimaji wa mionzi kwenye kahawa na utaratibu mzima wa upatikanaji wa vibali vya kusafirisha zao hilo nje ya nchi bila kutumia mawakala .
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Dennis Mwalongo amewaambia wafanyabiashara hao kuwa lengo la elimu waliyoipata ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kubakia katika soko la kahawa yenye ubora na isiyo na vimelea vya uchafuzi wa mionzi.
“Tunawaelewesha hapa sababu za kupima mionzi kwenye kahawa kwani ni muhimu sisi kama taasisi tuna wajibu wa kuhakikisha madhara yatokanayo na mionzi hayatokei,” amesema Mwalongo.
Sheria Na. 7 ya mwaka 2003 ya Nguvu za Atomiki Tanzani, imeipa mamlaka TAEC kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini.
Kutokana na hali hiyo, amesema TAEC itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara mbalimbali nchini juu ya kazi zake kwa lengo la kusaidia kutoa uelewa zaidi juu ya upimaji wa mionzi kwenye bidhaa mbali mbali zinazosafirishwa ndani na nje ya nchi.