KHARTOUM, SUDAN
SUDAN imetimiza mwaka mmoja tangu kuondolewa kwa Rais Omar al-Bashir. Lakini hakuna cha kusherehekea.
Uchumi bado uko dhaifu, hali ya kisiasa bado ni tete, huku janga la virusi vya corona likizusha mtafaruku mwingine.
Mwaka mmoja uliopita , mamia kwa maelfu ya raia wa Sudan walifanya maandamano ya wiki nzima mbele ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Mwanafunzi kijana mwanamke, Alla Salah, alisimama juu ya gari akiimba kauli mbiu za kisiasa, baadaye alikuja kuwa ishara ya vuguvugu la maandamano katika jamii ambayo kwa kiasi kikubwa inadhibitiwa na wanaume zaidi.
Kila mmoja aliingia mitaani, ikiwa ni pamoja na maprofesa, waalimu na madaktari.
Wasanii waliandika ujumbe na kuchora picha za uhuru katika kuta mjini Khartoum.
Kwa miezi kadhaa , nchi hiyo ilikuwa ikitokota hadi hatimaye kile ambacho hakikufikirika kikatokea.
Rais Omar al-Bashir alipinduliwa Aprili 11, 2019, baada ya kukaa madarakani karibu miaka 30.
Yalikuwa mapinduzi yaliyoelezwa na wengi kuwa ni vuguvugu la mapinduzi ya mataifa ya Kiarabu namba mbili.
Lakini mwaka mmoja baadaye, katika kusherehekea mwaka mmoja wa siku hii kubwa, hali mjini Khartoum imenyong’onyea.
Kwasababu ya janga la virusi vya corona, shule na vyuo vikuu vimefungwa. Sherehe za maadhimisho , kupeperusha bendera na kuimba wimbo wa taifa ama nyimbo za mapinduzi, vimefanyika nyumbani ama katika mitandao ya kijamii.
Lakini kuna sababu nyingine ya hali hiyo ya kunyong’onyea: Baada ya miezi 12 ya uhuru wa kisiasa , Sudan haijapiga hatua ambayo ilipigiwa matumaini.