29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yaibua taarifa mpya

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TANGU kuzuka kwa virusi vya corona (Covid-19) mwishoni mwa mwaka jana nchini China, kumekuwa na taarifa mpya karibu kila wiki kuhusu idadi ya watu wanaoambukizwa, vifo na zaidi tafiti zinazotoka kwa wanasayansi duniani.

Wakati baadhi ya nchi zikirekodi maambukizi mapya kila wiki, huku Marekani ikielekea kuongoza dunia kwa idadi ya vifo na maambukizi, wanasayansi sasa wamekwenda mbali na kuonya binadamu kuchukua tahadhari na wanyama wenye mwingiliano nao kama paka, mbwa, nyani na wengine.

Hatua ya wanasayansi hao imekuja baada ya wiki iliyopita duma kutoka eneo la kufugia wanyama la Bronx, New York nchini Marekani ambalo kwa sasa limefungwa tangu Machi 16 mwaka huu, kupimwa na kuonyesha kuwa na virusi vya corona.

Duma huyo jike mwenye miaka minne aliyebatizwa jina la Nadia, pamoja na wanyama wengine aina ya paka wakubwa inadhaniwa kwamba waliambukizwa na mtunzaji wa wanyama hao ambaye alikuwa na dalili za virusi vya corona.

Inaelezwa kuwa wanyama hao walianza kuonyesha dalili ikiwa ni pamoja na kifua kikavu mwishoni mwa mwezi uliopita.

“Hii ni mara ya kwanza kwa yeyote kati yetu kutambua mahali popote duniani kwamba mtu aliambukiza mnyama huyo na mnyama huyo akaugua,” Paul Calle, ambaye ni daktari mwandamizi wa wanyama alikaririwa na Shirika la habari la Reuters wiki iliyopita kabla ya taarifa za sasa.

Ingawa Shirika linalofuatilia afya za wanyama duniani na Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema hakuna ushahidi kwamba mbwa au paka wanaweza kuambukiza virusi vya corona, limesisitiza kuwa tafiti zaidi zitafanyika kufahamu jambo hilo, na kutoa rai kwa yeyote ambaye ni mgonjwa kutokuwa karibu na wanyama hao.

KINACHOFAHAMIKA KUHUSU CORONA NA WANYAMA 

Virusi vya corona vilibainika kwa mara ya kwanza katika eneo la Wuhan nchini China mwishoni mwa mwaka jana.

Vinasadikika vilitoka kwa wanyama na kuingia kwa binadamu kupitia soko la wanyama na viumbe hai la Wuhan.

Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kupitia ukurasa wake wa Sayansi limeandika kuwa virusi hivyo vimekuwa vikienea kwa binadamu kwenda kwa binadamu, lakini taarifa za wiki iliyopita kuhusu maambukizi ya  duma Nadia, zinaibua maswali mapya kuhusu maambukizi ya mwanadamu na wanyama.

Kabla ya taarifa hizo, huko nyuma mbwa wawili wa Hong Kong nao walibainika kuwa na virusi vya corona ingawa kumekuwa na ripoti chache kuhusu kuwatenga wanyama wanaoambatana na binadamu.

BBC imeandika kwamba wataalamu wa uhifadhi wameonya kuwa virusi vinaweza kuleta tishio kwa wanyama wengine wa porini kama nyani wakubwa na wamesema hatua zinahitajika kupunguza hatari.

HALI ILIVYO DUNIANI

Wakati taifa la China ambako ndiko chimbuko la ugonjwa huo kwa siku kadhaa likionekana kutoka kwenye maambukizi makubwa, jana tena limeripoti taarifa za maambukizi mapya ya watu 46 na hivyo kuibua sintofahamu.

Italia iliyokuwa ikionekana kuongoza kwa vifo vingi vinavyofikia 18,849, kuna kila dalili zinazoonyesha kuwa nafasi hiyo itachukuliwa na Marekani baada ya jana kuthibitisha vifo vya nchi nzima kufikia 18,780 huku wagonjwa 2,000 wakiripotiwa kupoteza maisha katika Jiji la New York ndani ya saa 24.

Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, ambacho kinafuatilia takwimu za ugonjwa huo kote duniani, Marekani inaongoza kwa wagonjwa wanaofikia nusu milioni (501,000).

Kutokana na hilo, katika moja ya uchambuzi wake, jarida la Forbes limeeleza kuwa kutakuwa na mabadiliko katika urari wa nguvu ya dunia, kwamba kiwango kitaongezeka zaidi kuelekea China na nchi za Asia zitaimarika kabla ya Marekani.

Hadi jana, idadi ya vifo duniani imefikia 104,000 huku watu walioambukizwa wakifika milioni 1.71 na zaidi ya 361,000  wakiripotiwa kupona virusi hivyo.

Aidha wakati pia ugonjwa huo  ukionekana tishio duniani kutokana na kasi ya maambukizi na vifo, daktari wa  nchini Uingereza, Amir Khan amechambua juu ya ugonjwa huo akisema watu wenye dalili za kawaida kama kifua kikavu na homa wanaweza kupona pasipo kupata madhara katika miili yao.

Hata hivyo, alisema wanasayansi sasa wanaamini kwamba ushahidi umeongezeka hasa kwa watu ambao wamekumbwa na shida kubwa ya kupumua na nimonia, kwamba wanaweza kubaki na madhara makubwa na ya muda mrefu kwenye mapafu na hata figo.

HALI YA NCHINI

Wakati hali ikiwa hivyo duniani, hapa nchini ndani ya wiki hii vifo vya watu wengine wawili vimeripotiwa juzi na kufanya jumla kufikia watatu.

Kuripotiwa vifo hivyo na ongezeko la wagonjwa wengine saba waliothibitika kuambukizwa virusi hivyo na kufanya jumla ya wagonjwa wote kufikia 32, kunaonyesha idadi ya maambukizi kupanda kila wiki.

Kesi za wagonjwa hao na watu waliopoteza maisha zimebainika ndani ya siku 25 tu tangu kisa cha kwanza kilipotangazwa nchini Machi 16, mwaka huu.

Taarifa hizo za ongezeko la wagonjwa zimekuja ikiwa imepita siku moja tu tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliposema maambukizi yanayotokea sasa ni ya ndani kwa ndani na kwamba hatua zisipochukuliwa, ndani ya siku chache watu wataanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe.

Jana Waziri Ummy hakutoa taarifa yoyote mpya kuhusu ugonjwa huo.

Lakini hatua ya kuwataja waliofariki dunia kwa ugonjwa huo ambao hadi sasa ni watatu na wote ni wanaume na wakazi wa Dar es Salaam, kumewafanya wengi kuchukua tahadhari. 

Kabla ya kutangaza ongezeko la vifo na wagonjwa hao, mapema wiki hii Ummy alitahadharisha umma hususani wakazi wa Dar es Salaam waangalie kama kuna umuhimu wa kwenda vijijini ili waangalie wasije wakawapelekea wazazi wao virusi hivyo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuna watu 280 wanaofuatiliwa baada ya kukutana na wagonjwa, huku wasafiri waliopo karantini wakiwa 120.

Hali kadhalika wagonjwa waliopona na kuruhusiwa wakiwa ni watano.

Wagonjwa 32 waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huo hadi sasa wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Kagera na Zanzibar.

Idadi ya wagonjwa 19 wanatoka katika Mkoa wa Dar es Salaam, tisa Zanzibar, wawili Arusha na mikoa ya Mwanza na Kagera ikiwa na mgonjwa mmoja mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles