China yapata maambukizi mapya 46 ya corona

0
664
Rais wa China, Xi Jinping

BEIJING, CHINA 

China jana iliripoti visa vipya 46 vya maambukizi ya corona, vikijumuisha 42 vya wasafiri kutoka nje ya taifa hilo ikiwa ni siku moja tu baada ya kutolewa ripoti ya visa vingine 42. 

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa kamisheni ya taifa ya afya ya China. 

Hadi kufikia jana idadi jumla ya maambukizi nchini humo inaonesha watu 81,953, wakati vifo vimeongezeka vitatu na kufanya jumla ya watu waliofariki kwa virusi hivyo kufikia 3,339.

Wakati huo huo Waafrika wanaoishi katika mji mkubwa kabisa wa kusini mwa China Guangzhou wamesema kuwa wanalengwa na mamlaka za eneo hilo, kwa kushukiwa na kuondolewa kwa nguvu majumbani mwao, kuwekwa katika karantini kwa nguvu na wengi kufanyiwa kwa pamoja vipimo vya virusi vya corona wakati nchi hiyo ikiimarisha vita dhidi ya maambukizi yanayotokana na watu wa kutoka nje. 

Mamlaka za eneo hilo la kiviwanda lenye idadi ya watu milioni 15 zimesema karibu watu 8 waliopatikana na virusi hivyo walikuwa katika wilaya ya Yuexiu, inayofahamika kama “Afrika Ndogo,” kutokana na idadi kubwa ya Waafrika wanaoishi hapo. 

Watano kati yao walikuwa raia wa Nigeria waliokumbana na hasira baada ya ripoti kuibuka kuwa walikiuka hatua ya lazima ya kujiweka katika karantini na walikuwa katika migahawa minne na maeneo mengine ya umma badala ya kubakia majumbani. 

Kutokana na hilo, karibu watu 2,000 waliokutana nao walihitajika kupimwa ugonjwa wa COVID-19 au kuwekwa katika karantini. 

Chombo cha habari cha serikali kimesema mji wa Guangzhou umethibitisha visa 114 vya virusi vya corona viliyosambazwa na watu kutoka nje ya nchi, ambapo kufikia Alhamisi wiki hii, 16 walikuwa Waafrika. Wengine walikuwa ni raia wa China.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here