NA JUSTIN DAMIAN |
PAMOJA na baadhi ya watu na mashirika ya kimataifa kupinga ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha megawati za umeme 2,100, mradi huu una umuhimu mkubwa kwa nchi.
Umuhimu wa mradi huu ni kwamba, kwanza utaweza kuzalisha umeme mwingi na pili umeme wa gharama nafuu na ni sehemu ndogo tu itaathirika ya asilimia tatu ya pori tengefu la Selous. Maji ndiyo chanzo pekee duniani ambacho kimethibitika kuweza kuzalisha umeme wa gharama nafuu.
Wakati mradi huu ukipata upinzani, Tanzania inatajwa kama moja kati ya nchi ambazo zina upatikanaji mdogo zaidi wa nishati ya umeme Afrika, ikiwa inakadiriwa kufikia asilimia 32, kwa mujibu wa Shirika la Power Africa.
Wazo la kujenga mradi huu ambao utazalisha umeme wa kutosha na wa gharama nafuu, ni wa kupongezwa na kuungwa mkono. Ukikamilika ni wazi kuwa bei ya umeme itashuka na kuleta nafuu kwa wananchi.
Pamoja na upinzani mkubwa, Tanzania imesisitiza uamuzi wake wa kuendelea na mpango wa kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji yaliyopo ndani ya Pori la Akiba la Selous.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi, alinukuliwa katika mkutano wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) ambao ulifanyika katika Jiji la Krakov nchini Poland, akisema Tanzania itajenga mradi huu.
Milanzi alikuwa akizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Urithi wa dunia kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Watanzania.
Katika mkutano huo, Tanzania ilipinga rasimu ya azimio Na. 41 COM 7 A. 17 aya ya 7 ambalo liliitaka kusitisha kabisa (to permanently abandon) ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Hydro Power Project).
Baada ya tamko la Tanzania kupinga azimio hilo, kipengele hicho kilifanyiwa marekebisho na neno la ‘kusitisha kabisa’ liliondolewa katika azimio hilo kupisha majadiliano zaidi.
Mradi kama huu unafanana na mradi uliojengwa katika mto Cuanza, nchini Angola wenye uwezo wa jumla ya megawatts 2,070 unaojulikana kama Laúca Hydropoer Plant (Mtambo wa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia maji ya mto wa Laúca) ambao upo mbioni kukamilika.
Mtambo wa Laúca ni mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia maji nchini Angola, ikiwa inazidi mitambo iliyokuwa imefungwa awali ya Capanda (520MW) na mtambo wa Cambambe (960 MW)”, kwa mujibu wa maelezo kutoka Odebrecht, ambayo ni kampuni inayoendesha mradi huo na inayowajibika katika uhandisi, manunuzi ya vifaa na huduma za ujenzi, ikijumuisha usambazaji, ukusanyaji na kuidhinisha mitambo yote ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa maelezo ya Odebrecht kampuni Ujenzi ya Brazil, generata la sita linafungwa na pindi litakapoanza kufanya kazi, Laúca itafikia uwezo kamili uliokusudiwa wa kuzalisha MW 2,070 na kuwa moja kati ya mitambo mikubwa zaidi ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia maji katika eneo la kusini mwa Afrika, sambamba na mtambo wa kuzalisha nishati kwa kutumia nguvu za maji wa Cabora Bassa uliopo Msumbiji.
“Kwa kuwa mtambo huu unaotoa nishati nafuu ya umeme na kuchangia katika kuimarisha mfumo wa umeme wa Angola, wakati huo huo mtambo wa uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji wa Laúca unaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini. Inatabiriwa kwamba hifadhi itaweza kufikia kiwango chake cha juu mwishoni mwa Aprili 2018, kwa kuhakikisha kwa kiwango cha usawa wa usalama-uwezo wa kusambaza nishati katika kipindi cha ukame kinachotarajiwa kutokea katika nusu ya pili ya mwaka,” inasema taarifa ya kampuni hiyo.
Mtambo wenye kiwango cha nishati sawa na Laúca utakaojulikana kama mtambo wa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji wa Stiegler’s Gorge wa Tanzania. (Stiegler’s Gorge Hydropower Plant) unatarajia kujengwa Julai mwaka huu, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati.
Historia ya mradi inaonesha wakati fulani wajenzi kutoka Brazil walikuja Tanzania na kuufanyia uchunguzi mradi wa Rufiji na kuondoka na hivyo kutoa picha kuwa kuna uwezekano wa Wabrazil hao kujenga mradi huo kwani unalingana na ule wa Angola.
Ujenzi katika mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ulioko katika hifadhi ya wanyama ya Selous, Unesco World Heritage site itatumia miezi 36 kukamilisha.
Kwa kujumuisha na vyanzo vya sasa vya uzalishaji wa umeme, mradi huu utaweza kuongeza uwezo wa sasa wa nishati ya umeme wa Tanzania kwa zaidi ya mara mbili ambayo ilikadiria kuwa ni 1,264MW kwa nchi nzima mwaka 2017.
Rasilimali kubwa ya gesi ya Tanzania na kuwepo kwa uwezekano wa kujengwa kwa vyanzo vya uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji ni vigezo vya msingi vitakavyosaidia nchi kufikia malengo yake katika kufikia upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wote kufikia mwaka 2030 kama malengo ya maendeleo endelevu yanavyotaka.