Ibada za Kanisa Katoliki zimefutwa kwa wiki ya pili katika mji mkuu wa Sri Lanka, Colombo. Serikali imeonya juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi zaidi kutoka kwa kundi lenye mafungamano na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS ambalo limehusishwa na mashambulio ya mabomu wakati wa sikukuu ya Pasaka.
Padri Edmund Tillakaratne, msemaji wa Parokia ya Colombo, amesema Kardinali Malcolm Ranjith amefuta ibada zote za Jumapili katika jimbo hilo kulingana na ripoti za usalama za hivi karibuni.
Waziri mmoja wa Sri Lanka amesema mawaziri wa serikali wanaweza kulengwa katika mashambulizi ya kigaidi. Wakati huo huo Polisi nchini humo jana jioni walichapisha majina na picha za watu tisa wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya siku ya Pasaka kwenye makanisa na hoteli za kitalii yaliyosababisha kuuwa watu wapatao 253.