32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SPIKA AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA ALMASI

NA KULWA MZEE-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametekeleza mapendekezo ya Rais Dk. John Magufuli kwa kuunda kamati ya wajumbe tisa, maalumu kwa ushauri kuhusu mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini.

Ndugai alisema hayo kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti na kuongeza kwamba ameunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu.

“Kamati  itakuwa na wajumbe tisa, itaongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu na itafanya kazi kwa siku thelathini kuanzia Julai 10, mwaka huu.

“Kamati itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini, kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini.

“Wajumbe wa Kamati ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Dk. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti maalumu (CCM) Shally Raymond, Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Restituta Mbogo, Mbunge wa Wawi Ahmed Juma Ngwali (CUF).

“Wajumbe wengine ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM) ambaye atakuwa Mwenyekiti,” alisema Ndugai.

Alisema wajumbe hao wameteuliwa kwa kuzingatia vigezo vya taaluma, uzoefu, pande za Muungano, jinsia na uwakilishi wa vyama vya siasa bungeni.

Ndugai alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa siku thelathini kuanzia Julai 10 na kituo kikuu cha kazi kitakuwa katika Ofisi ya Bunge Dodoma na itakapobidi, kamati itafanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia muda wake wa kazi, bajeti na ulazima wa kufanya ziara hizo na itakapobidi itafanya ziara nje ya nchi.

Alisema hadidu za rejea za kamati hiyo kuwa ni kuchambua taarifa za tume na kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na Serikali kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini na kuona mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na Serikali.

Nyingine ni kutathmini mfumo uliopo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini ya almasi nchini na kubainisha manufaa ambayo Serikali inapata kutokana na uwekezaji uliopo katika madini hayo.

Spika Ndugai alisema hadidu rejea nyingine ni kushughulikia jambo jingine lolote linalohusu mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa madini ya almasi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles