SIRRO: KIBITI SASA NI UBAYA UBAYA

0
839
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, akionyeshwa gari na Mkuu wa Mipango wa Kampuni ya Kifaru, Mario Gasparri wakati alipokabidhiwa magari manne ya msaada kutoka Kampuni ya Haval Motors, Dar es Salaam jana kwa ajili ya matumizi ya hilo jeshi la polisi. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, akionyeshwa gari na Mkuu wa Mipango wa Kampuni ya Kifaru, Mario Gasparri wakati alipokabidhiwa magari manne ya msaada kutoka Kampuni ya Haval Motors, Dar es Salaam jana kwa ajili ya matumizi ya hilo jeshi la polisi. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi

Na Waandishi Wetu,

KIBITI sasa ni ubaya, ubaya. Hayo ni maneno ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro.

Amesema wanaotekeleza mauaji dhidi ya raia katika eneo hilo, wametumwa vibaya na wao watapelekwa vibaya vibaya.

Sirro alisema hayo jana Dar es Salaam kabla ya kukabidhiwa magari manne na Kampuni ya Great Wall Motor and Haval Company kutoka nchini China yatakayotumiwa na jeshi hilo.

“Tatizo la mauaji ya raia huko Kibiti na maeneo mengine nchini, nataka kusema si kawaida yangu kuongea sana, ila sio muda mrefu yatakwisha, hadi sasa tunakwenda vizuri na wale ambao wametumwa kutekeleza mauaji hayo wataona majibu yake.

“Sisi Watanzania hatujazoea vurugu za namna hii sasa kama wametumwa, wametumwa vibaya na sisi kama Jeshi la Polisi tutakwenda nao vibaya vibaya, cha msingi tunaomba ushirikiano kwa wananchi,” alisema Sirro.

Pia aliwataka viongozi wa vijiji na Serikali za mitaa nchini kote kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kukabiliana na wimbi la uhalifu.

Tangu wahalifu kuanza kutekeleza mauaji kwenye maeneo ya Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani, zaidi ya watu 30 wamefariki dunia wakiwamo askari polisi zaidi ya 10, viongozi wa Serikali za vijiji na kata.

Jeshi la Polisi limekuwa likiendesha operesheni maalumu kwenye eneo hilo na mara kadhaa limetangaza kupambana na wahalifu hao na kufanikiwa kuua baadhi yao. 

MAGARI YALIYOKABIDHIWA

Kuhusu magari aliyokabidhiwa Sirro, alisema yatasaidia katika kukabiliana na kupunguza changamoto zilizopo za kiuhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Great Wall Motor and Haval, Jianguo Liu, alisema magari hayo yatasaidia Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla katika suala zima la kiuhalifu.

“Haval ni kampuni inayohusika na kutengeneza magari nchini China, hivyo kutokana na changamoto tulizoona pamoja na ushirikiano wetu wa muda hapa Tanzania, tumeamua kutoa magari haya ili yasaidie kukabiliana na tatizo hilo,” alisema Liu.

Naye Kamishna wa Jeshi la Polisi – Fedha na Usafirishaji, Albert Nyamhanga, alisema kila gari moja thamani yake ni Dola za Marekani milioni 57.

 ALIYEJERUHIWA KWA RISASI KIBITI ANG’OLEWA JICHO

Wakati huohuo, madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamelazimika kumfanyia upasuaji na kuondoa jicho la kulia kijana Michael Martin (28), ambaye alijeruhiwa kwa risasi huko Kibiti.

Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake, Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Neema Mwangomo, alisema Martin alifanyiwa upasuaji huo Juni 29.

“Tulimpokea Martin na kumlaza hapa hospitalini tangu Juni 28, mwaka huu akitokea Hospitali ya Mchukwi iliyopo Kibiti, alikuwa amejeruhiwa kwa kupigwa risasi katika jicho lake la kulia,” alisema.

Mwangomo alisema madaktari walimfanyia uchunguzi wa awali na kubaini kwamba jicho hilo lilikuwa tayari limepasuka.

“Walichunguza pia jicho lake la kushoto na kubaini mishipa ya fahamu ilikuwa imepata majeraha. Baada ya uchunguzi ndipo wakashauri wamfanyie upasuaji wa kuliondoa kabisa jicho la kulia na kumwanzishia dawa maalumu kulitibu jicho la kushoto ambalo limejeruhiwa pia,” alisema.

Alisema Martin bado amelazwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu na akiuguza kidonda chake.

“Kwa sasa hali yake ni nzuri, imeanza kuimarika na madaktari kila wakati wanakwenda kumwona na kumpatia matibabu,” alisema.

 Habari hii imeandaliwa na MANENO SELANYIKA, VERONICA ROMWALD na SAID ABDALLAH (OUT)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here