24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta aliongoza mgomo chuo kikuu

samwelNa LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

WASOMI mbalimbali waliozungumza na MTANZANIA kwa nyakati fofauti Dar es Salaam jana, wamemwelezea Spika wa zamani wa Bunge Samuel Sitta kuwa na kusema kuwa atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya wakati wa uhai wake ikiwamo kuongoza mgomo wakati akiwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhadhiri katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Josephat Kanywanyi, alisema Sitta atakumbukwa kwa uvumilivu na kutoa nafasi kwa wapinzani wakati alipokuwa Spika wa Bunge.

Profesa Kanywanyi alisema alikutana na Sitta wakiwa wanasoma sheria UDSM.

“Nilimfahamu Sitta mwaka 1966 tulipokuwa tunasoma hapa chuoni (UDSM) kabla sijaondoka kwenda nchini Marekani kwa masomo, nikiwa huko nikasikia chuo kimefungwa kwa mgomo na yeye akisimamishwa, hakutakiwa kurudi kutokana na kutajwa kuwa aliongoza mgomo, nadhani wakati huo alikuwa mwaka wa pili.

“Mwaka 1970 alirudi kuendelea na masomo mwaka wa tatu na wakati huo nami nilikuwa nimerudi nimeanza kufundisha hapa. Kwa kweli alikuwa kijana mchangamfu, shupavu na mshiriki mzuri wa mijadala ya siasa ya chuo na alikuwa mahiri darasani, kama inavyofahamika wakati huo chuo kilikuwa kinapokea wanafunzi wenye uwezo mkubwa” alisema mhadhiri huyo.

Alisema kuwa Sitta alitumia ujuzi mkubwa kama mbunge na Spika na alionyesha umahiri katika kuliongoza Bunge na kulifanya kuwa chombo cha kuheshimika kama mhimili unaojitegemea na alilifanya kutekeleza majukumu yake ya kutunga sheria na kanuni vizuri.

Prof. Kanywanyi alisema kuwa hata alipokuwa Spika, Sitta alionyesha kitu cha ziada kwa vyama vya upinzani kwa kuruhusu Serikali kupata mawazo mbadala kwa kukosolewa, hivyo anapaswa kukumbukwa kwa hilo.

Hata akiwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alifanya kazi nzuri ya kulisimamia na kutuletea rasimu ya katiba japo yako mambo mengine aliyafanya ambayo hatukuyategemea, nadhani yalitokana na mambo ya chama chake,” alisema Prof. Kanywanyi.

Alisema kuwa taifa limepoteza mtu mahiri na mwenye uelewa mkubwa wa kina katika masuala ya sheria.

“Sitta atakumbukwa pia kwa mchango mkubwa alioutoa katika kukiendeleza Kituo cha Uwekezaji (TIC) alipokuwa akifanya kazi katika kituo hicho pamoja na mchango wake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuweka misingi imara ya kuiendeleza alipokuwa Waziri wa Afrika Mashariki,” alisema.

Mhadhiri mwingine, Dk. Benson Bana wa UDSM, alisema kuwa Sitta alipandisha hadhi ya Bunge na kuziwezesha kamati za Bunge kuwa na nguvu ya kufanya uamuzi kwa kuishauri na kuikosoa Serikali pale ilipokosea.

Aidha Dk. Bana alisema kuwa Sitta atakumbukwa daima kwa kuanzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).

“Mbali na kuziwezesha kamati, pia alitetea masilahi ya wabunge na kijisimamia mwenyewe katika kamati mbalimbali, hakusubiri kusukumwa. Hata katika kashfa ya Richmond na EPA alionyesha umahiri mkubwa uliozaa matokeo ya waziri mkuu wa wakati huo Edward Lowassa kujiuzulu,” alisema Dk. Bana.

Alisema kuwa Sitta hakuwa mtu wa kunyamazia mambo, alikuwa mwenye msimamo, alipinga vitendo vya rushwa kwa kauli zake alizokuwa akizitoa.

“Kwa ujumla alikuwa mtu mwenye kuanzia katika familia ambako alifanikiwa kumshawisi mkewe kuingia katika siasa na kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi,”alisema.

Mke wa Sitta, Magrethi Sitta ni Mbunge wa Urambo Mashariki, jimbo alilolishikilia mumewe hadi 2015.

“Tuyaendeleze aliyoyaacha na kuyaishi yale aliyoyatenda, hakuwa mwoga. Hata aliopokuwa hapa (UDSM) aliweza kuwashawishi wenzake kugoma, wakati wa mwalimu (Nyerere) haikuwa rahisi mtu kumpinga kwa yale aliyoyaagiza, lakini Sitta hakuogopa,” alisema Dk. Bana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles