Na ZAINAB IDDY
KWA takribani misimu minne sasa, Klabu ya Simba imekuwa ikipiga kelele juu ya timu za Yanga na Azam kuwa na mechi nyingi za viporo.
Simba kupitia kwa viongozi wake wanadai timu hizo kuwa na mechi nyingi za viporo, kunatokana na hila za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutopanga ratiba ya ligi vizuri ili kuzibeba timu hizo mbili.
Aliwahi kukaririwa Msemaji wa Simba, Haji Manara, akisema hawapo tayari kuingiza timu uwanjani kama wapinzani wao wa jadi, Yanga watakuwa hawajakamilisha mechi za viporo katika ligi ya msimu huu.
Ni kauli ya kishujaa, lakini haina mantiki kutokana na ukweli kuwa, Yanga na Azam haziwezi kuvikwepa viporo, labda kama TFF kupitia Bodi ya Ligi itaamua kusimamisha ligi kipindi ambacho timu hizo zipo kwenye kuliwakilisha Taifa, jambo ambalo halitaweza kutokea kwa soka la Tanzania.
Inafahamika wazi kuwa, Azam na Yanga, ndizo zinazoiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), inayotarajiwa kuanza Februari, mwakani, ikiwa Yanga wakikipiga katika Klabu Bingwa, huku Azam FC wakituwakilisha Kombe la Shirikisho.
Timu hizi mbili zimekuwa katika ushiriki wa mashindano hayo zaidi ya miaka mitatu sasa, huku ushiriki huo ukichangia uwepo wa ‘viporo’ vingi katika ligi ya nyumbani kwa timu hizo.
Tukitupia jicho katika ligi za wenzetu, hususan nchi za Misri, Zambia, Afrika Kusini na kwingine, utagundua kuwa michezo ya viporo ipo, tena ni mingi zaidi ya ilivyokuwa kwa ligi ya Tanzania Bara.
Iangalie Zamalek, ilifika fainali CAF mwaka huu, ilikuwa na michezo zaidi ya mitano ya viporo, tupia jicho Zesco waliofika hatu ya nusu fainali klabu bingwa, angalia Mamelod Sundowns ambao ndio mabingwa wa Afrika, hadi sasa wanaendelea kucheza michezo ya kiporo Ligi Kuu Afrika Kusini, lakini hakuna timu iliyogomea kucheza wala kupiga kelele juu ya viporo vyao kwa kuwa wanajua ni vipi wanabeba dhamana ya nchi yao kimataifa.
Ufike wakati Simba wafahamu viporo kwa washindani wao katika kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara haviepukiki, hivyo wataendelea kuumia na kusononeka kama tu wasipokubaliana na hali hiyo, huku dhana ya kwamba TFF inazibeba timu fulani ikiendelea kutawala vichwani wao.
Tuchukulie iwapo timu za Yanga na Azam watafika hatua ya 16 bora- watalazimika kucheza kwa mtindo wa makundi, iwe isiwe, michezo ya viporo itakuwepo, ikizingatiwa itakuwa katika mzunguko wa pili, utakapowasikia Mtaa wa Msimbazi wakitokwa povu na hata kugomea michezo.
Inafahamika wazi soka la Afrika halifanani na lile la Ulaya, ambalo Simba wanatolea mfano, hivyo mzunguko wa pili mechi za viporo hazitaweza kukwepeka na kizuri zaidi msimu huu Wanajangwani wameweka mahesabu ya kutwaa ubingwa, sina shaka watafanikiwa, tunasubiri kuona iwapo wataweza kukwepa suala la kuwa na viporo kwenye ligi.
Kiroho safi inasema iwapo Simba haitakuwa tayari kubadili mtazamo hasi walionao juu ya hilo, basi sitashangaa kuona wakitokwa povu kwa viporo vya Yanga na Azam kwa mara nyingine.