27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

UMRI ULIVYOTIA DOSARI LIGI YA VIJANA

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


kikosi-cha-azamKWA mara ya kwanza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeweza kuanzisha ligi ya vijana wenye umri  chini ya miaka 20 kwa kuvihusisha vikosi vya pili vya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mashindano hayo yalianza Novemba 15, mwaka huu, kwa hatua ya makundi, ikifanyika kwenye vituo viwili ambavyo ni Chamanzi cha jijini Dar es Salaam na kile cha Bukoba, mkoani Kagera, mechi ikichezwa dimba la Kaitaba.

Katika mashindano hayo ya vijana, timu 16 shiriki ziligawanywa kwenye makundi  mawili, ambapo kituo cha Bukoba, Azam ndiyo iliyoongoza baada ya kumaliza mechi za makundi ikiwa na pointi 17, wakati kituo B cha Dar es Salaam, Simba imeweza kuibuka kidedea ikiwa na pointi sawa na Azam.

Kumalizika kwa hatua hiyo ya makundi kunatoa nafasi kwa timu mbili kila kundi kusonga hatua ya nusu fainali, kabla ya kuchezwa fainali na kumpata bingwa wa ligi ya vijana msimu wa 2016/17.

Hata hivyo, pamoja na kufanyika kwa mara ya kwanza, mashindano hayo yaliyochukua nafasi ya Uhai Cup, iliyofanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2013, bado msisimko umeonekana kuwa mdogo, huku sababu mbalimbali zikitajwa kuchangia.

SPOTI KIKI imepata nafasi ya kuzungumza na viongozi na makocha wa timu shiriki, lakini pia wachambuzi wa soka, kila mmoja kwa nafasi yake akizungumzia changamoto zilizojitokeza na kipi kifanyike kwa ajili ya kuboresha ligi hiyo msimu ujao.

Kocha wa kikosi cha Yanga, Wanne Mkisi, anasema katika kituo cha Bukoba changamoto kubwa ilikuwa ni suala la umri, jambo lililosababisha kutotimia kwa malengo ya kuanzishwa kwa ligi hiyo na TFF.

Anasema katika mechi zilizocheza timu yake dhidi ya Stand United, Mbao, Kagera  na Mwadui, ilijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na wapinzani wao kuonekana wana umri mkubwa zaidi ya wale wa Yanga.

“Kiukweli kwa mwaka huu lengo la TFF la ligi ya vijana chini ya miaka 20, halijatimia kwa kuwa wenzetu kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wameonekana kuwatumia wachezaji waliokuwa juu ya umri uliowekwa, jambo lililosababisha mara kwa mara vijana wangu kujikuta wakipata majeraha na hili nililigundua kutokana na kuwa na tofauti kubwa pindi tulipocheza na Azam,” anasema Mkisi.

Naye mratibu wa timu ya Majimaji, Mohamed Sebene, anasema licha ya changamoto ya umri iliyoonekana wazi, lakini timu nyingi zilikuwa zikishiriki mashindano hayo katika hali ngumu, kutokana na ukata uliokithiri mifukoni mwao.

“TFF inatakiwa kuangalia jinsi ya kuziwezesha timu shiriki, kwani safari hii tumeshiriki katika hali ngumu kiasi cha kutoa mwanya kwa baadhi yetu kufanya vitendo vinavyoashiria wameuza mechi, hivyo iwapo mwakani yatafanyika ni vizuri kwanza likaboresha suala la udhamini, ndipo unaweza kupatikana ushindani wa kweli, tofauti na mwaka huu,” anasema Sebene.

Kwa upande wa Philip Alando, ambaye ni Meneja wa Azam, anasema TFF imejitahidi kulingana na uchumi wao na hali halisi ya ugumu wa fedha iliopo sasa.

“Mashindano haya yamefanyika kwa mara ya kwanza, hivyo changamoto hazikosekani, ikiwemo katika suala la waamuzi kushindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo, udanganyifu wa umri na mengineyo ambayo kama yatafanyiwa kazi tunaweza kufikia lengo la kuanzishwa ligi ya vijana,” anasema Alando.

Upande wa kocha wa kikosi cha Simba, Nicolaus Kiondo, anasema kwanza anaipongeza timu yake kufika hatua ya nusu fainali ikiwa haijapoteza mchezo, lakini pia anawaunga mkono TFF kwa kuanzisha ligi ya vijana ambayo ina faida kubwa kwenye soka la Tanzania.

Kwa upande wa changamoto, anasema: “Kubwa ni suala la umri, kwani kuna baadhi ya wachezaji wanaonekana kuzidi miaka 20 iliyowekwa, lakini pia kutotenda haki kwa waamuzi kutokana na kushindwa kutafsiri sheria za soka, vitu ambavyo vinaweza kurekebishika iwapo TFF itaviwekea mkazo,” anasema.

Wachambuzi nao wanena

Oscar Oscar ni miongoni wa wachambuzi wa soka mahiri hapa Tanzania, ambaye anatoa pongezi nyingi kwa TFF kutokana na kuanzisha ligi hiyo, licha ya changamoto kadha wa kadha zilizojitokeza ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi kabla ya kuchezwa tena mwakani.

Oscar anasema mwaka huu wa kwanza kwa ligi hiyo, jambo kubwa lililoonekana kuwa na mapungufu ni kutokuwepo kwa vitu muhimu vya kiafya, ikiwemo gari la kubeba wagonjwa pamoja na madaktari waliobobea katika kutoa huduma kwa wanamichezo.

“Licha ya kwamba gari la wagonjwa, madakatri na ulinzi viwanjani kuwa ni jukumu la mmiliki wa uwanja, lakini TFF ilipaswa kufanya ukaguzi iwapo vitu muhimu vipo mahali wanapopeleka mashindano yoyote.

“Kuhusu suala la umri linalolalamikiwa, TFF hawastahili kubeba lawama hizo, kwa kuwa wao kazi yao kubwa ni kuandaa sera na kuifikisha kwa watekelezaji ambao ni timu shiriki, huku wakiamini wanachama wao watazifuata kanuni na taratibu za mashindano zilizowekwa, kitendo cha viongozi kuwapeleka watu waliovuka umri uliotakiwa ni kushindwa kuzitekeleza sheria zilizowekwa.

Anasema: “Kutokana na malalamiko yaliyojitokeza kwa baadhi ya timu juu ya umri mkubwa wa washiriki, inawapasa klabu kuwa na mikakati ya kuwapata vijana kwa kuwatengeneza, wakianzia katika umri wa chini  kama ilivyofanya Azam, ili kutoenda kinyume na matarajio ya TFF, ukizingatia mashindano haya yanatakiwa kusapotiwa kwa nguvu zote yanaweza kusaidia kukuza soka la Tanzania iwapo kila mmoja kwa nafasi yake akifanya kazi kiuweledi”.

Naye kocha mahiri na mchambuzi wa soka, Kenedy Mwaisabula ‘Mzazi’, anaungana na Oscar kuipongeza TFF kwa kuanzisha ligi hiyo, lakini akizitaka timu shiriki kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Anasema: “Licha ya mapungufu yaliyojitokeza, lakini bado TFF inahitajika kuungwa mkono kwa kuanzisha jambo lenye manufaa ya soka la Tanzania, ingawa watu wachache wanafanya vitu vinavyokwenda kinyume cha matarajio ya mashindano hayo.

“Kwanza tunatakiwa kuwapongeza TFF kwa jambo hili zuri na pia kuwashauri kipi kifanyike ili kuweza kupata udhamini utakaoweza kuongeza chachu ya mashindano, bila kusahau kupiga vita na kufichua uovu wa baadhi ya timu zinazokwenda kinyume cha kanuni na sheria za mashindano zilizowekwa,” anasema Mwaisabula.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles