28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya ushindi Azam hadharani

AZNA OSCAR ASSENGA, TANGA

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, amesema mabadiliko ya staili ya uchezaji wa kikosi hicho kwa asilimia kubwa ndio siri ya ushindi waliopata juzi dhidi ya Mgambo Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania.

Katika mchezo huo wa kuhitimisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao Mgambo.

Staili mpya ya kupiga mipira mirefu inayoweza kulifikia lango la wapinzani kwa urahisi, ndio ubunifu na mbinu mpya za makocha wa Azam ambao wamegundua unaweza kusaidia kupatikana kwa ushindi katika viwanja wa ugenini.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kitambi ambaye ni msaidizi wa Mwingereza Stewart Hall, alisema walilazimika kubadilisha staili ya uchezaji iliyozoeleka kutokana na mazingira ya uwanja waliokuwa wakiutumia.

Alisema ushindi huo utazidi kuwapa presha wapinzani wao Yanga ambao wanapigana kwenye kinyang’anyiro cha kushika usukani wa ligi na kudai kuwa Azam inajiamini kutokana na ubora wa kikosi chake, hivyo wataendelea kupambana hadi mwisho wa ligi msimu huu.

“Unajua tunapocheza katika viwanja vya ugenini ni tofauti sana na tunapoutumia uwanja wetu wa nyumbani wa Azam Complex, hivyo ni lazima tubadilishe aina ya uchezaji kwa kupiga mipira mirefu,” alisema.

Kitambi alisema anaamini hiyo ndio silaha pekee inayoweza kuwasaidia kupata ushindi wanapocheza katika viwanja vya ugenini ambavyo mazingira yake hayafanani na uwanja wao.

Kocha huyo aliongeza kuwa dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi zinazofuata ili malengo yao ya kuendelea kuongoza ligi yaweze kutimia na hatimaye kutwaa ubingwa ambao kwa sasa unashikiliwa na Yanga.

“Malengo yetu ya msimu huu ni kuhakikisha tunachukua ubingwa jambo ambalo halina ubishi, kwani tunazidi kujipanga na kujiimarisha ili tushinde mechi zote zinazofuata na kufikia mafanikio hayo,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles