24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI YA MAJAJI KUACHA KAZI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


HATUA ya majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuacha kazi kwa wakati mmoja imezua mjadala.

Moja ya jambo kubwa lililojitokeza kuhusu hatua hiyo, ni tuhuma za kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, huku mwingine ikielezwa ni mgonjwa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, ilisema Rais Dk. John Magufuli ameridhia maombi ya kuacha kazi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Jaji Aloysius Mujulizi.

Mwingine ambaye Rais Magufuli ameridhia kuacha kwake kazi, ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Upendo Msuya na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, huku kilichowafanya kuacha kazi kikiwa hakijaelezwa.

“Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, imeeleza kuwa Rais Magufuli amekubali maombi ya kuacha kazi kwa viongozi hao kuanzia Mei 15, 2017,” ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wamehusisha kuomba kuacha kazi kwa Jaji Mujulizi, kuwa kunatokana na kashfa ya Escrow, wakisema amesoma alama za nyakati.

Jaji Mujulizi ni mmoja wa vigogo waliotajwa kupokea mgawo wa Sh milioni 40.4 kutoka kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, uliotokana na fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Jumla ya Sh bilioni 321 ziliwekwa katika akaunti hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kusubiri suluhu ya kesi yake na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Siku chache baada ya kuibuliwa kwa kashfa hiyo, Rugemalira aliyekuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL, alisema kati ya fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo, alilipwa Dola za Marekani milioni 75 sawa na Sh bilioni 120  ambazo aliziita ‘vijipesa vya ugoro’.

Baadhi ya fedha hizo, aligawia watu mbalimbali wakiwamo majaji, wanasiasa na viongozi wa dini.

Wakati taarifa ya Ikulu juu ya Jaji Mujulizi na wenzake kuomba kuacha kazi ikitolewa jana, hivi karibuni tu wakati wa maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alihoji sababu ya Serikali kutotekeleza maazimio ya Bunge, ikiwa ni pamoja ya yale ya Escrow.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema atakaa na Spika kujua maagizo ambayo utekelezaji wake bado.

Pia alisisitiza kuwa mengine hayajatekelezwa kwa sababu yalikuwa yanahitaji uchunguzi zaidi.

Kwa upande wake, Jaji Msuya pamoja na mambo mengine, taarifa ambazo gazeti hili halijaweza kujiridhisha usahihi wake, zinasema ni mgonjwa.

Inaelezwa hadi jaji afikie uamuzi wa kuacha kazi, kuna mambo makuu matatu yanayopaswa kuwapo, ambayo ni kustaafu, ugonjwa na kukaa pembeni kupisha tume ya kimahakama kufanya uchunguzi wa jambo fulani.

 

Maoni

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, alisema kitendo cha jaji huyo kuomba kuacha kazi, inawezekana kuna shinikizo nyuma yake.

“Inawezekana kuna shinikizo nyuma yake… kama Serikali hii mpya imeamua kupambana na ufisadi na ukizingatia huko nyuma kashfa kubwa za ufisadi kama EPA hazikushughulikiwa, inawezekana Rais Magufuli ameamua kulishughulikia hili,” alisema Profesa Mpangala.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema jambo kubwa analoliona kwa majaji hao wawili kuacha kazi, inaweza ikatokana na mhimili wa mahakama kutokuwa na Jaji Mkuu.

Alisema kutokuwapo kwa Jaji Mkuu kunayumbisha mhimili huo na hata majaji wengine katika utendaji wa kazi zao.

 “Mahakama ni mhimili muhimu wa kusimamia haki, sasa inapoongozwa na Kaimu Jaji Mkuu haileti picha nzuri… Je, Rais yeye kama mkuu wa nchi angekuwa rais wa muda angejisikiaje?

“Pamoja na sababu nyingine inayotajwa kwa Jaji Mujulizi kuwa ni kutokana na kashfa ya Escrow,” alisema Profesa Baregu.

 

Dawa za kulevya

Wakati akikabidhiwa majina 97 ya wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya, Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, alisema kuna mahakimu na majaji ambao wamekuwa wakivuruga kesi za watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Kutokana na hilo, alisema watapitia kesi zote za dawa za kulevya ili kuwabaini na kisha watapeleka orodha kamili katika mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

“Kesi ambazo zilivurugwa na mahakimu na majaji, ushahidi ulikuwa wazi kuwa mtuhumiwa amemeza dawa za kulevya, hakimu akasema mtuhumiwa alikuwa na matatizo ya vidonda vya tumbo,” alisema Kamishna Sianga.

Akihutubia sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari, mwaka huu, Rais Magufuli alionekana kukerwa na utendaji wa vyombo vya haki na dola unaosababisha Serikali ipoteze mapato.

Pia alieleza kushangazwa na jinsi mahakimu 28 walioshtakiwa kwa makosa ya rushwa mwaka jana, lakini wote wakashinda kesi zao jambo ambalo alisema linaibua maswali kuhusu utendaji kazi wa vyombo vya dola na utoaji haki za mahakama.

Katika hilo, alidokeza kuna majaji wengi walienda mapumziko nje ya nchi kwa kujigharamia, huku wanne tu kati yao wakilipiwa na Serikali.

“Unajua maneno haya ninayozungumza ni magumu sana kuzungumzwa kwa majaji, kwa sababu leo hii nikitoka mnaweza mkawa mmeshakitafuta kipengele. Na huwa mna kipengele cha mtu kusema huyu ameshindwa kutawala kwa sababu akili yake haikuwa normal (kawaida),” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles