30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU YACHUNGUZA VIGOGO ELIMU

NA PATRICIA KIMELEMETA


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza kuwachunguza vigogo wa elimu waliosimamishwa kazi kwa ajili ya uwapo wa vitabu feki vya shule za msingi na sekondari vyenye makosa.

Vigogo hao, ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk. Elia Kidga na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolaus Buretta.

Akizungumza na MTANZANIA,Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Takukuru, Musa Misalaba alisema taasisi hiyo ilianza kazi tangu vigogo hao walipopewa barua ya kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.

Alisema kutokana na hali hiyo, upelelezi wa suala hilo unaendelea na  litakapokamika wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Suala la vigogo wa elimu limeshatua Takukuru, tayari tumeanza kulifanyia uchunguzi, hatuwezi kulizungumzia kwa undani tutaharibu upelelezi, tusubiri  ukamilike,”alisema Misalaba.

Alisema baada ya kukamilika upelelezi huo, upelelezi utawasilishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Elimu, John Kalage alisema wanaunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuwasilisha viongozi hao na kufanya uchunguzi wa vitabu hivyo.

Alisema mara nyingi taasisi hiyo, imekuwa ikiwaeleza viongozi wa Serikali uwapo wa vitabu feki ambavyo vimechangia kushusha hadhi ya elimu, lakini wameshindwa kuchukua hatua wala kufanya uchunguzi wa jambo hilo, hali iliyochangia wanafunzi kuendelea kuvisoma wakati havina ubora unaohitajika.

Alisema vitabu hivyo vimeigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha, kuanzia  uchapishaji hadi usambazaji shuleni, jambo ambalo linapaswa kukemewa siyo kwa wadau wa sekta ya elimu peke yao, bali na Watanzania wote kwa sababu wameisababishia hasara Serikali.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali inahitaji kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja na namna ya kupata vitabu bora ambavyo vitakaguliwa na watalaamu wa fani ya elimu kabla ya kusambazwa kwenye shule  kwa ajili ya kufundishia.

“Ni kweli vitabu feki vipo… na tuliwahi kuwaambia viongozi juu ya suala hili walishindwa kuchukua hatua, badala yake viliendelea kusambazwa kwa ajili ya wanafunzi kusoma na kufundishiwa, huku fedha zinazotumika ni za serikali.

“Ifike wakati Serikali ishirikishe wadau mbalimbali wa serkta ya elimu kwa ajili ya kutoa maoni yao ya nini kifanyike ili kuhakikisha tunapata vitabu bora ambavyo vitatumika kwa ajili ya kusoma na kufundishia wanafunzi wetu, jambo ambalo linaweza kuchangia kuwapo kwa elimu bora,”alisema Kalage.

Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi waliowajibika wamebeba msalaba wa watendaji wengine.

“Ukiwa kiongozi unapowajibika unabeba msalaba wa wengine lazima tukubali ukweli baadhi ya vitabu wanavyosoma wanafunzi shuleni vina makosa,”alisema.

Alisema Serikali inapaswa kuwa makini na haina ya vitabu vinavyofundishwa shuleni kwa sababu idadi kubwa havina ubora kwenye ngazi mbalimbali hadi ya uhariri.

Nayo Taasisi ya Utafiti ya Twaweza, imesema haijawahi kufanya utafiti juu ya uwapo vitabu feki, hivyo haiwezi kuliongelea suala hilo kwa undani.

Katika kikao cha Bunge kilichofanyika juzi mjini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alitangaza kuwasimamisha kazi vigogo hao ili kupisha uchunguzi wa suala hilo .

Pamoja na hayo, Profesa Ndalichako alisema viongozi wengine watawajibika baada ya kufanyika uchunguzi, kuwa  ni pamoja na waliohusika wakati wa kuhariri na kuandika maudhui ya vitabu hivyo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles