29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI NZITO BARUA KWA KKKT

Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam           |       


KITENDO cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, kujitokeza hadharani na kudai barua ya Serikali iliyoandikwa kwenda Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ni batili, kimeibua maswali mengi.

Miongoni mwa maswali hayo ni mtu aliye nyuma ya kusudio la kuandikwa kwa barua hiyo, ambaye Mwigulu amekwishatangaza kuwa anachunguzwa.

Pia lengo na utaratibu uliotumiwa kuiandaa na kuiwasilisha kwa uongozi wa Kanisa la KKKT ambao umekiri kuwa uliipokea kwa kusaini kitabu maalumu (dispatch), lakini na wao kuwasilisha majibu yao kwa mfumo huo huo mapema wiki hii.

Lakini pia kama barua hiyo haikuandikwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Msajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, swali linabaki kuwa aliyeiandika alipata wapi ujasiri huo wa ajabu na hata kughushi nembo na sahihi.

Pamoja na kwamba Mwigulu ametangaza kumsimamisha na kumchunguza Komba ambaye naye ni miongoni mwa wanaodaiwa kuandika barua hiyo, lakini kitendo cha kutoweka wazi jibu lake sasa iwapo amehusika au la, nacho kimeibua maswali na hata kujenga hisia tofauti miongoni mwa watu wanaofuatilia suala hilo.

Godfrey Lyatuu ambaye amejitambulisha kwenye gazeti hili kama mfuatialiji wa masuala mbalimbali ya kijamii, alisema Mwigulu alipaswa kueleza kabla ya uchunguzi alichowajibu Komba.

“Angewaeleza waandishi wa habari hicho alichowajibu baada ya kumuuliza kwenye vikao vyao vya ndani na kama wameamua kumchunguza angesema hatujaridhishwa na majibu yake haya na haya ndiyo maana tumeamua kumchunguza, vinginevyo hili linazua maswali na kuacha sintofahamu kama barua ile ilikosa baraka,” alisema.

Watu waliofuatilia mwenendo mzima wa tukio hilo, walisema iwapo uchunguzi utabaini kama Komba aliandika barua hiyo, basi naye huenda huko mbele ya safari akalazimika kujibu maswali mengine mengi zaidi.

Maswali hayo ni pamoja na iwapo kama aliandika barua hiyo kwa ridhaa yake kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Msajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii.

Jingine kama aliandika ni kwanini alikiuka utaratibu na hata kushindwa kushirikisha watendaji wengine kama kuacha nakala kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, wala kwa Waziri au Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Pia atalazimika kujibu kile kilichomsukuma kuandika barua hiyo sasa, ilihali miongoni mwa mambo ambayo barua hiyo ilitaka KKKT ifute, ni waraka wake wa Pasaka uliotoka Machi 24 mwaka huu, takribani miezi miwili iliyopita.

Kama hakuhusika, alichukua hatua gani baada ya kuona jina na sahihi yake imetumika katika barua hiyo na hata kusubiri hadi Waziri aitishe mkutano na waandishi wa habari na kisha kutangaza kumsimamisha na kumchunguza.

ASKOFU ATOA KAULI NZITO

Wakati maswali hayo yakizuka sasa, mmoja wa maaskofu wa KKKT aliyezungumza na MTANZANIA Jumapili, alisema hata kama barua hiyo ingekuwa si batili, wasingekuwa tayari kufuta waraka wao wa Pasaka, ambao pamoja na mambo mengine ulionya mwenendo wa nchi katika masuala ya uchumi, siasa na kijamii.

“Tusingekuwa tayari kukanusha waraka ule ambao uliandaliwa na maaskofu 27, tusingefanya hivyo kabisa, kwa sababu kanisa linaongozwa na lina taratibu zake ambazo zimo kwenye katiba yake… maaskofu ni viongozi wa kanisa,” alisema askofu huyo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kuwa si msemaji.

Akizugumzia tamko la Mwigulu kumsimamisha kazi Komba, lakini pia kufuatilia ilipotoka barua hiyo, askofu huyo alisema lilikuwa na matobo mengi.

Alihoji sababu za Mwigulu kumsimamisha Komba kama barua hiyo haijatoka kwenye ofisi yake.

Juzi katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao Dk. Mwigulu alitangaza kumsimamisha kazi Komba ili kupisha uchunguzi, aliwataka maaskofu na viongozi wa dini walioguswa na barua hiyo kuipuuza, akisema Serikali inaheshimu uhuru wa watu kuabudu na kwamba mambo ya dini si ya kuguswaguswa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles