NEW YORK, Marekani
LICHA ya staa wa vipindi vya Keeping up with the Kardashian, Kim Kardashian (35), kuhofia video, picha na vitu vyake mbalimbali vya siri kuanikwa hadharani baada ya moja kati ya simu zake mbili kuibiwa, mrembo huyo pia anaweza kupoteza zaidi ya dola milioni moja kwa mwezi kutokana na kutokutupia vitu vyake katika mitandao yake ya kijamii.
Kabla ya simu zake zenye vitu vingi hazijaibiwa alipovamiwa hotelini Paris nchini Ufaransa, Kim alikuwa akiingiza zaidi ya dola milioni moja kila mwezi kutokana na kutupia video, picha na matukio yake mbalimbali kwenye mitandao yake ya kijamii.
“Kwa ‘brand’ ya Kim inatengeneza dola milioni moja kwa mwezi kwa kuposti tu vitu vyake, lakini havihusiani na mikataba mingine kati yake na kampuni nyingine anazofanya nazo kazi,” alieleza mshauri wake wa masuala ya fedha, Samuel Rad.
Samuel aliongeza kwamba mrembo huyo anaweza kupoteza dola 20,000 kwa ‘brand’ yake ambazo ni sawa na zaidi ya milioni 40 za Tanzania kwa kutokuposti mambo yake binafsi ambayo hayaingiliani na malipo yake ya zaidi ya dola milioni moja atakazozikosa.
“Natumaini kitu atakachokipost kwa mara ya kwanza baada ya mkasa wake wa kuvamiwa na kuibiwa kitapata wafuatiliaji wengi na kitaleta manufaa makubwa, inabidi apate usaidizi kwa kitu atakachokuja kukipost ili kililete hamasa na manufaa kwake kwa kuteka vyombo mbalimbali vya habari,” alieleza Samuel.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi la Ufaransa lipo mbioni kuwatia nguvuni walioiba vito vya thamani ya zaidi ya dola milioni 11 vya Kim Kardashian, baada ya kukuta baadhi ya vito nje ya hoteli aliyokuwa Kim, mke wa mwanahip hop, Kanye West (39) wenye watoto wawili North (3) na Saint miezi 10 alipokuwa amevamiwa.
Kwa mujibu wa Daily Mail, polisi watatumia kipimo cha vinasaba (DNA) kutoka katika vito hivyo ili kuwatambua wavamizi hao wanaodaiwa kufanya kosa la kuangusha baadhi ya vito walivyoibiwa.